Rais Samia ashiriki Mkutano wa UN uliojadili Mabadiliko ya Tabia nchi mjini New York

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Septemba 20, 2021 ameshiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliojadili athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba Dunia na kusisitiza umuhimu wa kutopuuzia juhudi za kukabiliana na janga hilo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akitoka katika Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa UN Jijini New York Nchini Marekani Septemba 20,2021, baada ya kushiriki mkutano uliojadili masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi.

“Tuko katika kipindi ambacho wakati tunapambana na athari za Mabadiliko ya Tabia Nchi bado tunataabika na changamoto kubwa ya sasa ambayo ni Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO – 19 ambayo imeangusha sana hali ya uchumi na kufuta mafanikio yaliyokwishafikiwa katika miongo kadhaa ya kujenga jamii zetu;

Rais Samia amesisitiza pia kuwa ingawa watu wengi wanachukulia kirahisi kupanda kwa hali ya joto kama moja ya athari za mabadiliko ya Tabia Nchi, bado hali ni ya kusikitisha kwa nchi kama Tanzania kwani hali hiyo husababisha ukame ambao ni athari mbaya kwa sekta zinazotegemea maliasili kama vile kilimo, uvuvi na misitu ambazo zinachangia asilimia 30 ya pato la Taifa na kuathiri takribani asilimia 60 ya wananchi.

Mkutano huo ambao ni mfululizo wa mikutano ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 26 wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi (COP26) utakaofanyika Glasgow, Uskochi mwezi Novemba, 2021, umejadili hatua za upatikanaji fedha kwa ajili ya kugharamia ustahimilivu na upunguzaji wa athari za mabadiliko ya Tabia Nchi.

Washiriki katika mkutano huo pia wamejadili umuhimu wa kutilia mkazo hatua dhidi ya Mabadiliko ya Tabia Nchi yanayoikumba dunia kwa kuwa athari zake na uharibifu wa mazingira hupunguza kasi ya nchi katika ukuaji kiuchumi na hata kuhatarisha usalama wa nchi.

Mkutano huo ni moja ya mikutano mahsusi inayofanyika katika Kilele cha Mkutano wa 76 wa Umoja wa Mataifa ambao kauli mbiu yake ni “Kujenga ustahimilivu kupitia matumaini – kuondokana na UVIKO – 19, kufanyia kazi mahitaji ya Ulimwengu, kuheshimu haki za watu na kuboresha Umoja wa Mataifa”.

Wakati huo huo, Rais Samia pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Comoro, Azali Asoumani na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Rebecca Nyandeng Garang.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na Rais wa Comoro, Mhe. Azali Assoumani, walipokutana jijini New York Nchini Marekani Septemba 20, 2021.

Viongozi hao wamezungumzia kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na mataifa hayo.

Mhe. Rais Samia ameelekeza kufanyika haraka kwa mikutano ya Tume za kudumu za ushirikiano baina ya mataifa hayo ili kuangalia namna ya kuboresha zaidi mahusiano.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makamu wa Rais wa Sudan Kusini, Mhe. Rebecca Nyandeng De Mabior, walipokutana Jijini New York Nchini Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi UNHCR Bw. Filippo Grand, walipokutana jjini New York nchini Marekani Septemba 20,2021. (PICHA NA IKULU).

Aidha, Mheshimiwa Rais Samia amefanya mazungumzo na Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ambapo viongozi hao wamezungumzia kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Shirika hilo hususan katika kusaidia wakimbizi walioko nchini Tanzania.

Filippo Grandi ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kubeba mzigo mkubwa wa wakimbizi kwa takriban miongo sitasasa ambapo pia amependekeza kuwepo na mkutano katika ngazi ya wataalam baina ya UNHCR, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Mambo ya Nje ili kuondoa changamoto katika kuwahudumia wakimbizi.

Rais Samia ameelekeza kikao hicho kufanyika mara moja ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa nje ya Ukumbi wa mikutano wa Umoja wa Mataifa UN Jijini New York Nchini Marekani Septemba 20,2021, baada ya kushiriki mkutano uliojadili masuala ya Mabadiliko ya Tabia Nchi. Kulia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula. Kushoto ni Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani,Balozi Kennedy Gaston.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news