RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUENDELEZA KILIMO NCHINI-MAJALIWA

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili kuhakikisha nchi inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula na ziada kuuza nje.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata melezo kutoka kwa Service Man, Costantine Magina (kushoto) kuhusu uoteshaji wa miche ya michikichi wakati alipotembelea shamba la kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Bulomboa Mkoani Kigoma, Septemba 16, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ameyasema hayo leo Septemba 16, 2021 baada ya kukagua shamba la michikichi la kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) 821 KJ Bulombora akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Kigoma.

Amesema Serikali inatekeleza dhamira hiyo kwa kufuatilia kwa ukaribu kilimo cha mazao hayo likiwemo na la michikichi kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa shamba hadi upatikanaji wa pembejeo. “Wazazi waanzishieni watoto wenu mashamba ya michikichi kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi ili wasiwe tegemezi.”

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi hususani waliopo kwenye mikoa inayolima michikichi washiriki katika kilimo cha zao hilo kwa ajili ya kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla. “Wekezeni katika kilimo cha michikichi kwa ajili ya maendeleo yenu pamoja na watoto wenu.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali imeamua kulipa kipaumbele zao hilo ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini. Amesema Serikali inatumia zaidi ya sh. bilioni 400 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi, hivyo ufufuaji wa zao hilo utaliwezesha Taifa kuzalisha mafuta ya kutosha.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama miche ya michikichi wakati alipokagua kitalu cha miche katika shamba la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Bulombora mkoani Kigoma, Septemba 16, 2021. Wa pili kulia ni Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu amewasisitiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Kigoma waratibu vizuri kilimo hicho ikiwa ni pamoja na kuwa na kanzidata itakayoonesha idadi ya wakulima, ukubwa wa mashamba yao na maeneo wanayolima ili kurahisisha utoaji wa huduma.

Amesema baada ya Serikali kupata mafanikio katika mazao ya biashara ya korosho, tumbaku, pamba, kahawa na chai, sasa imeamua kuongeza mazao mengine ya michikichi, mkonge, zabibu na parachichi ili nayo yaweze kuzalishwa kwa wingi na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa na kambi yake ya Bulombora kwa kuitikia wito wa kulima zao la michikichi kwa vitendo na kwamba shamba hilo linatarajiwa kuwa la mfano kwa kilimo cha zao hilo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama miche ya michikichi wakati alipokagua kitalu cha miche katika shamba la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Bulombora mkoani Kigoma, Septemba 16, 2021. Kulia ni Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama miche ya michikichi wakati alipokagua kitalu cha miche katika shamba la michikichi la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Bulombora mkoani Kigoma, Septemba 16, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Mabele amesema katika kambi hiyo wamepanga kupanda ekari 2,000 za michikichi kwa awamu, ambapo mwaka jana walipanda ekari 500 na mwaka huu wanatarajia kupanda eneo jingine la ukubwa wa ekari 500.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news