Rais Samia atoa Bilioni 2.6- ujenzi Kituo cha Magari Nyakanazi

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kituo cha kimkakati cha maegesho ya magari makubwa katika eneo la Nyakanazi wilayani Biharamulo, Kagera.
Ameyasema hayo leo Septemba 18, 2021 wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Nyakanazi baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho ambao unagharimu sh. bilioni 2.6 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2021.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa kuwaagiza viongozi wa Mkoa wa Kagera wahakikishe wanasimia vizuri miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ukiwemo na huo wa ujenzi wa kituo cha maegesho ya magari makubwa kwa maendeleo ya wananchi.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kuhakikisha eneo la Nyakanazi linapimwa na kuanisha matumizi ya kila eneo ikiwemo makazi, Huduma za Jamii, Viwanda, Viwanja vya Michezo na maeneo mbalimbali ya uwekezaji
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Nyakahura wilayani Ngara akiwa njiani kuelekea Ngara, Septemba 18, 2021. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).

Kwa upande wake, Mhandisi wa TARURA wa wilaya ya Biharamulo, Julius Sumaye ambaye ndiye msimamizi wa ujenzi wa mradi huo amesema unalengo la kuongeza mapato ya halmashauri ili iweze kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu.

Amesema halmashauri yao imetenga eneo la ukubwa wa hekta 10 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya uwekezaji ambapo kati yake hekta 3.2 zimetumika katika ujenzi kituo hicho, hekta 2.3 ni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi na hekta 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya biashara.

Mhandisi huyo amesema kwa awamu ya kwanza wameanza na ujenzi wa mradi wa kituo cha kuegeshea magari makubwa chenye uwezo wa kuegesha malori 300 kwa wakati mmoja. Mradi huo umefikia asilimia 48 ya utekelezaji wake

Post a Comment

0 Comments