RMO Tanga: Uchanjaji Awamu ya Pili utakuwa na mafanikio

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Jonathan Budenu amesema uchanjaji wa Awamu ya Pili ya chanjo ya UVIKO 19 utafanyika kwa mafanikio, kwani umelenga kutoa elimu ya kutosha kuanzia kwa wananchi, viongozi mbalimbali ikiwemo wa dini, utamaduni na kimila.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Basilla Mwanukuzi (wa pili kushoto) akiongoza kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwa Halmashauri ya Wilaya (DC) na Halmashauri ya Mji (TC). (Picha na Yusuph Mussa).

Lakini pamoja na makundi hayo, pia wahudumu wa afya ngazi ya halmashauri ikiwemo kwenye hospitali, vituo vya afya na wafanyakazi wa afya kwenye jamii (Community Health Workers- CHW) watapata elimu hiyo, hivyo kuwa rahisi katika utekelezaji wa chanjo hiyo.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipofika kwenye kikao cha Afya ya Msingi (PHC) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe (DC) na Halmashauri ya Mji Korogwe (TC) ambacho kilikuwa kinapanga namna ya kuanza zoezi la uchanjaji Awamu ya Pili chini ya Mwenyekiti wake, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basilla Mwanukuzi.

Dkt. Budenu alikiri, uchanjani wa Awamu ya Kwanza wa UVIKO 19 haukuwa na maandalizi, na hiyo ni kutokana na uharaka, hasa ukichukulia UVIKO 19 ni janga la kidunia. Kwa kuliona hilo, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya TAMISEMI, imetoa fedha ili kufanikisha zoezi hilo kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali.
Wajumbe wa kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwa Halmashauri ya Wilaya (DC) na Halmashauri ya Mji (TC). (Picha na Yusuph Mussa).

"Ni kweli uchanjaji wa kwanza haukuwa na mafanikio makubwa sababu watu hawakuandaliwa katika chanjo ya UVIKO 19. Na hiyo ni kutokana na uharaka wa jambo hilo. Lakini sasa Serikali imejipanga, na zoezi hilo litashirikisha watu wengi ikiwemo wahudumu wa afya wenyewe katika kupata elimu, kuna vikundi vya ngoma, waandishi wa habari, wazee maarufu, wananchi, viongozi wa dini na makundi mengine" alisema Dkt. Budenu.

Naye Mwanukuzi alitaka Kamati hiyo kwa kushikiana na wadau wengine waweze kufanya kazi kwa ubunifu na mbinu mbadala kuona wanawaaminisha wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama. Ni baada ya wananchi kuwa na mtazamo mbaya kuhusu chanjo hiyo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RMO) Dkt. Jonathan Budenu akizungumza na Wajumbe (hawapo pichani) wa kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi (PHC) kwa Halmashauri ya Wilaya (DC) na Halmashauri ya Mji (TC). (Picha na Yusuph Mussa).

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Miriam Cheche alisema wao walipata chanjo 3,000, na hadi sasa zimetumika 1,000, hivyo wamejipanga kuona wanafanikisha zoezi hilo kwa chanjo 2,000 zilizobaki zinamalizika. Na ili kufanikisha hilo, watawashirikisha wadau mbalimbali kuona zoezi hilo linafanikiwa. Na kuongeza kuwa watatumia hadi Chanjo Mkoba kufika kusikofikika magari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news