Serikali yaunda timu maalumu kuchunguza kupanda bei ya mafuta, Waziri Mkuu atoa neno

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu maalumu ili kuchunguza kupanda kwa bei ya mafuta kwa kuwa kitendo hicho kinawaumiza wananchi hususan wale wa hali ya chini.
Amesema Serikali imechukua uamuzi huo baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati nchini (EWURA) kutangaza bei mpya elekezi ya mafuta kwa mwezi Septemba ambapo ilionesha kupanda kwa bei za bidhaa hizo. EWURA ilitangaza bei hiyo tarehe 31 Agosti, 2021.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo leo Ijumaa, Septemba 10, 2021 wakati wa kuahirisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 12 jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi tarehe
2 Novemba, 2021.

Amesema kufuatia tangazo hilo la kupanda kwa bei za bidhaa hizo, Septemba Mosi, 2021, Serikali ilisitisha bei mpya zilizotangazwa na EWURA ili kufanya mapitio ya kina ya kupanda huko kwa bei na siku iliyofuata iliunda timu ya uchunguzi.

“Pamoja na mambo mengine timu hiyo inafuatilia kupanda kwa bei za bidhaa za mafuta mara kwa mara hususani petroli, dizeli, mafuta ya taa na ndege na kisha itaishauri Serikali hatua stahiki za kuchukuliwa.”

Mbali na uchunguzi huo wa kupanda kwa bei, pia Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza timu hiyo ijiridhishe kuhusu utitiri wa tozo uliokithiri kwenye bidhaa za mafuta na itoe mapendekezo ya namna nzuri ya kushughulikia suala hilo.

“Mheshimiwa Spika napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa timu hiyo tayari imeanza kutekeleza majukumu yake tangu tarehe 2 Septemba, 2021. Hali kadhalika, itakapokamilisha taarifa yake Serikali itatoa mwelekeo wa yale yatakayopendekezwa.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari, Serikali imetumia shilingi bilioni 33.73 kwa ajili ya kujenga maboma 2,699 kati ya maboma 4,539 ya vyumba vya madarasa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Fedha hizo zinatokanana tozo ya miamala ya simu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka 2021, makadirio yanaonesha kuwa wanafunzi 934,706 sawa na asilimia 83.68 ya wanafunzi 1,115,041 waliohitimu mtihani wa darasa la saba wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari, 2022.

“Mheshimiwa Spika nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tayari Serikali imepeleka shilingi bilioni saba kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 560 ikiwa ni awamu ya kwanza. Aidha, maboma 1,840 yatakayogharimu shilingi bilioni 23 yatakamilishwa kupitia ruzuku ya Serikali Kuu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kurejea maelekezo aliyoyatoa wakati alipofungua mafunzo elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwamba wahakikishe wanakamilisha kwa wakati miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.

Amesema lengo la Serikali ni kuona vijana wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wanapokelewa na kuanza masomo yao kwa wakati. “Tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi bila Ada kumekuwa na mwitikio mzuri wa mahudhurio ya wanafunzi na hivyo kuongeza idadi ya wahitimu katika mitihani ya kujipima na kumaliza elimu ya msingi.”

“Ongezeko hilo la idadi ya wahitimu, lilisababisha changamoto ya kutokuwepo kwa miundombinu ya elimu ya kutosha hususan madarasa ya kuweza kupokea wahitimu wa darasa la saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.”

“Kufuatia hali hiyo, Serikali ilitoa maekelezo kwa watendaji wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatumia takwimu zilizopo kupanga maoteo na kutenga fedha katika mipango na bajeti ya kila mwaka ili miundombinu ya elimu, samani na shule hitajika viwepo kwa wakati.”
 
 
 
 

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA NNE WA BUNGE LA 12 LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TAREHE 10 SEPTEMBA, 2021 – DODOMA

 

Shukrani

 

1.           Mheshimiwa Spika, leo hii tunafikia tamati ya Mkutano wa Nne wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza kikao chake cha kwanza tarehe 31 Agosti, 2021. Hivyo, hatunabudi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa kwenye mkutano huu tukiwa buheri wa afya.

 

2.           Mheshimiwa Spika, vilevile, ninakushukuru wewe binafsi kwa kumudu kuliongoza vema Bunge hili tukufu, ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge. Aidha, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri mliyoitoa kwa kusema na kwa maandishi wakati wa kuchangia hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Serikali kwenye mkutano huu.

 

3.           Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa, Serikali kwa upande wake ipo tayari muda wote kupokea michango yenu yenye lengo la kusaidia kuboresha utekelezaji wa mipango yake.

 

Salamu za Pole

 

4.           Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kukupa pole kufuatia taarifa za kuhuzunisha za kifo cha Mheshimiwa Elias John Kwandikwa aliyekuwa Mbunge wa Ushetu na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kilichotokea tarehe 2 Agosti, 2021. Aidha, natoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote wa Jimbo la Ushetu kwa kuondokewa na mwakilishi wao huyo.

 

5.           Mheshimiwa Spika, vilevile, natoa salamu za pole kwa Kamanda Simon Nyakoro Siro, Inspekta Jenerali wa Polisi kufuatia tukio lililotokea tarehe 25 Agosti, 2021 jijini Dar es Salaam, ambapo askari wetu wazalendo wapatao watatu na mlinzi mmoja wa kampuni binafsi waliuawa wakati wakitekeleza majukumu yao ya kiusalama. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema na awape uponyaji wa haraka majeruhi wa tukio hilo. Amin!

 

6.           Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole Watanzania wenzangu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na wengine kupata ulemavu katika matukio mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani zilizogharimu maisha ya maafisa watano wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), waliofariki dunia tarehe 23 Agosti, 2021 wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi mkoani Songwe. Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahala pema peponi. Amina!

 

SHUGHULI ZA BUNGE

 

Maswali na Majibu

7.           Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu wa 4 wa Bunge la 12, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya msingi 119 na maswali 263 ya nyongeza ambayo yalijibiwa na Serikali. Kadhalika, maswali 14 ya papo kwa papo yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Waziri Mkuu.

 

Maazimio ya Bunge

 

8.           Mheshimiwa Spika, vilevile, Waheshimiwa Wabunge walijadili na kupitisha maazimio mawili ya Bunge kama ifuatavyo: -

Moja:      Azimio la Bunge kuhusu kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula (East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary – SPS Measures);

 

Mbili:      Azimio la Bunge kuhusu kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA); na

 

9.           Mheshimiwa Spika, kuridhiwa kwa maazimio haya kutasaidia nchi yetu kuimarisha biashara na uwekezaji kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki sambamba na kuongeza shughuli za biashara na uwekezaji wa ndani baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. Halikadhalika, kutaiwezesha Tanzania kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Afrika.

 

Miswada ya Sheria

 

10.        Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pia, walijadili na kupitisha miswada mitano ya sheria iliyowasilishwa na Serikali katika mkutano huu kama ifuatavyo: -

 

Moja:      Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2 wa Mwaka 2021;

 

Mbili:      Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.4 wa Mwaka 2021;

 

Tatu:       Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa Mwaka 2021;

 

Nne:        Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mwaka 2021. Marekebisho haya pia yanakusudia kuhakikisha shughuli za zimamoto na uokoaji nchini zinafanyika kwa ufanisi ili kuendelea kuwavutia wawekezaji kwa kuwahakikishia usalama wa maisha na mali zao; na

 

Tano:      Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.5 wa Mwaka 2021.

 

11.        Mheshimiwa Spika, nirejee tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao mizuri iliyotolewa wakati wa kujadili Miswada hiyo muhimu ambayo itasaidia kuondoa mapungufu yaliyobainika sambamba na kuboresha baadhi ya masharti katika utekelezaji wa sheria hizo. Serikali itafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa sheria hizo unawanufaisha Watanzania.

 

12.        Mheshimiwa Spika, niwapongeze na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri ya kuwasilisha Miswada iliyojadiliwa katika mkutano huu pamoja na kutoa ufafanuzi mbalimbali wakati wa kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Aidha, nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu wake kwa kazi nzuri ya kuandaa miswada iliyowasilishwa katika mkutano huu.

 

MAENEO YA MSISITIZO KISEKTA

13.        Mheshimiwa Spika, jukumu langu la msingi lililonisimamisha mbele ya Bunge lako tukufu ni kutoa maelezo mafupi hususan kuhusu shughuli za mkutano huu wa nne wa Bunge kabla ya kuahirishwa. Hata hivyo, kabla ya kuhitimisha mkutano huu naomba niweke msisitizo wa baadhi ya masuala kwa viongozi, watendaji na wananchi kwa ujumla katika kutekeleza majukumu yao ya kuwaletea maendeleo.

 

14.        Mheshimiwa Spika, baadhi ya maeneo ambayo nitayatolea msisitizo ni suala la tozo na uendelezaji wa miundombinu ya afya ya msingi, maandalizi ya uandikishaji wa wanafunzi wa kidato cha kwanza Januari 2022, matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, ujenzi wa Mji wa Serikali, tahadhari dhidi ya UVIKO-19 na michezo.

 

UENDELEZAJI WA MIUNDOMBINU YA AFYA YA MSINGI

15.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Afya ya Mwaka 2007 yenye lengo la kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa vituo vya afya na zahanati. Azma ya Serikali ni kuona kila kata inapata kituo cha afya na kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kusogeza huduma hizo karibu na wananchi na kuwaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu. Hadi sasa, tarafa 363 zilizopo Tanzania Bara zina vituo vya afya vyenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za dharura, huduma za mionzi na maabara za kisasa.

 

16.        Mheshimiwa Spika, ili kuzifikia tarafa nyingi zaidi, Serikali imeamua, kwanza kuzitambua kata za kimkakati na tarafa zote ambazo hazina vituo vya afya. Pili, kutumia fedha zitokanazo na tozo za miamala ya simu kujenga vituo vya afya vya kimkakati ambavyo vitakuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji za dharura, huduma za mionzi na maabara za kisasa katika kata za kimkakati na makao makuu ya tarafa hizo.

 

17.        Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imepeleka shilingi bilioni 37.5 zilizotokana na makusanyo ya tozo ya miamala ya simu kwenye Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye tarafa 150 kati ya tarafa 207. Kila kituo cha afya kimepelekewa shilingi milioni 250 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo. Natoa maelekezo kwa watendaji wote wa Serikali za Mitaa kuhakikisha fedha hizo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuakisi thamani ya fedha kwenye utekelezaji wa miradi hiyo.

 

MAANDALIZI YA UANDIKISHAJI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA KWANZA, JANUARI 2022

18.        Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu kwamba jana tarehe 9 Septemba, 2021 vijana wetu wa darasa la saba walimaliza mtihani wa Taifa wa Elimu ya Msingi ulioanza tarehe 8 Septemba, 2021. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwaombea Mwenyezi Mungu awajalie wote wafaulu vizuri na kujiunga na kidato cha kwanza, vyuo vya ufundi na kujiendeleza na taaluma nyinginezo.

 

19.        Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi bila Ada kumekuwa na mwitikio mzuri wa mahudhurio ya wanafunzi na hivyo kuongeza idadi ya wahitimu katika mitihani ya kujipima na kumaliza elimu ya msingi. Ongezeko hilo la idadi ya wahitimu, lilisababisha changamoto ya kutokuwepo kwa miundombinu ya elimu ya kutosha hususan madarasa ya kuweza kupokea wahitimu wa darasa la saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.

 

20.        Mheshimiwa Spika, kufuatia hali hiyo, Serikali ilitoa maelekezo kwa watendaji wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatumia takwimu zilizopo kupanga maoteo na kutenga fedha katika mipango na bajeti ya kila mwaka ili miundombinu ya elimu, samani na shule hitajika viwepo kwa wakati.

 

21.        Mheshimiwa Spika, maelekezo hayo, yalilenga kuiwezesha Serikali kutambua mahitaji ya miundombinu ya elimu yatakayokidhi idadi hiyo ya wanafunzi na hivyo kuhakikisha miundombinu hiyo inaandaliwa mapema. Katika mwaka 2021, makadirio yanaonesha kuwa wanafunzi 934,706 sawa na asilimia 83.68 ya wanafunzi 1,115,041 waliohitimu mtihani wa darasa la saba wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari, 2022.  

 

22.        Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari, Serikali imetumia shilingi bilioni 33.73 kwa ajili ya kujenga maboma 2,699 kati ya maboma 4,539 ya vyumba vya madarasa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Fedha hizo zinatokana na tozo ya miamala ya simu.

 

23.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tayari Serikali imepeleka shilingi bilioni saba kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 560 ikiwa ni awamu ya kwanza. Aidha, maboma 1,840 yatakayogharimu shilingi bilioni 23 yatakamilishwa kupitia ruzuku ya Serikali Kuu.

 

24.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kurejea maelekezo niliyoyatoa wakati nikifungua mafunzo elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwamba wahakikishe miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati. Lengo la Serikali ni kuona vijana wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wanapokelewa na kuanza masomo yao kwa wakati.

 

BEI ELEKEZI YA MAFUTA

 

25.        Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Agosti, 2021 Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati nchini (EWURA) ilitangaza bei mpya elekezi kwa bidhaa za mafuta kwa mwezi Septemba ambapo ilionesha kupanda kwa bei za bidhaa hizo. Kufuatia taarifa hiyo, na malalamiko ya wananchi juu ya kupanda kwa bei za bidhaa hizo, tarehe 1 Septemba 2021, Serikali ilisitisha bei mpya zilizotangazwa na EWURA ili kufanya mapitio ya kina ya kupanda huko kwa bei.  

 

26.        Mheshimiwa Spika, tulichukua hatua hizo kutokana na ukweli kwamba kupanda kwa bei ya mafuta huwaumiza wananchi hususan wale wa hali ya chini. Kwa kulitambua hilo, tarehe 2 Septemba, 2021, niliunda timu maalumu ya uchunguzi.

 

27.        Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengine timu hiyo inafuatilia kupanda kwa bei za bidhaa za mafuta mara kwa mara hususani petroli, dizeli, mafuta ya taa na ndege na kisha kuishauri Serikali hatua stahiki za kuchukuliwa. Aidha, nimeielekeza timu hiyo ijiridhishe kuhusu utitiri wa tozo kwenye bidhaa za mafuta na kuja na mapendekezo ya namna nzuri ya kushughulikia suala hilo.

 

28.        Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa timu hiyo tayari imeanza kutekeleza majukumu yake tangu tarehe 2 Septemba, 2021. Hali kadhalika, itakapokamilisha taarifa yake Serikali itatoa mwelekeo wa yale yatakayopendekezwa.

 

MFUMO WA STAKABADHI ZA MAZAO GHALANI NA USHIRIKA

29.        Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo ambayo Serikali inayapa msukumo wa kutosha ni masoko na mifumo ya mauzo ya mazao ya wakulima. Serikali inachukua hatua hizi ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata tija na kunufaika na mazao yao. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imeondoa mifumo isiyo rasmi ya ununuzi wa mazao ambayo imekuwa ikiwakandamiza wakulima na kuwanufaisha baadhi ya wanunuzi wasiokuwa waaminifu. Mathalan, tuliondoa mifumo kama vile kangomba, butula, chomachoma, kula maua, njemke na mingineyo ambayo ilikuwa ikimpunja na kumnyonya mkulima.

 

30.        Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo, Serikali imekuwa ikisimamia kikamilifu mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani ambao umeonesha mafanikio makubwa katika uuzaji wa mazao yakiwemo korosho, ufuta, dengu, choroko na kakao. Kwa lugha nyingine, ufanisi wa mfumo huo, umekuwa kichocheo katika kupunguza umaskini na kuongeza uchumi wa nchi na wakulima kwa ujumla.

 

31.        Mheshimiwa Spika, taarifa zinaonesha kuwa kuuza mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na ushirika kunatoa nguvu ya pamoja kwa wakulima katika upatikanaji wa masoko sambamba na kuimarisha bei ya mazao husika. Minada iliyofanyika imesaidia kuongezeka kwa bei ya mazao yaliyotumia mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwemo korosho, ufuta, dengu, choroko na kakao.

 

32.        Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 bei ya choroko iliongezeka kutoka shilingi 600 kwa kiwango cha chini hadi 800 kiwango cha juu kwa kilo na kufikia shilingi 900 hadi 1,300 kwa kilo katika vituo vya Magu, Uzogele, Igunga na Manyoni. Kadhalika, hivi karibuni tumeona bei ya kakao ikiongezeka maradufu kutoka shilingi 2,500 hadi 5,000 kwa kilo baada ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani.

 

33.        Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, natoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kushirikiana kwa karibu na vyama vya ushirika na vyama vya msingi katika kuhakikisha wanawawezesha wakulima kupata elimu na manufaa ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani bila usumbufu ili uwapatie tija.

 

34.        Mheshimiwa Spika, ni kweli mfumo wa stakabadhi ghalani unahitaji miundombinu ya maghala. Hata hivyo, changamoto hizo zinaendelea kufanyiwa kazi ili mazao mengi zaidi yaingizwe kwenye mfumo huo mwaka hata mwaka na kuleta tija zaidi kwa wakulima.

 

35.        Mheshimiwa Spika, rai yangu kwa wakulima na wanunuzi wa mazao ni kwamba, mfumo wa stakabadhi ghalani ndiyo pekee uliothibitika na kuonesha matokeo makubwa yenye manufaa. Hivyo basi, tuendelee kuuimarisha katika mazao yote ya biashara nchini ili kuleta mafanikio kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.

 

UNUNUZI WA NAFAKA NCHINI

36.        Mheshimiwa Spika, Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya chakula hususan nafaka pamoja na mazao ya biashara. Ongezeko hili la uzalishaji linakwenda sambamba na jitihada za Serikali za kuimarisha masoko ya ndani ya mazao pamoja na kutafuta masoko ya nje.

 

37.        Mheshimiwa Spika, pamoja na kuboresha mifumo ya masoko, Serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda vya uchakataji wa mazao yanayozalishwa hapa nchini ili kuimarisha bei ya mazao hayo na hivyo kumpatia tija mkulima.

 

38.        Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa mahindi hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, tulipokea malalamiko ya wananchi kuhusu umbali wa vituo vya kununulia mahindi na bei kutoridhisha. Kama mnavyofahamu, kwa kiasi kikubwa ununuzi wa mahindi nchini hufanywa na wafanyabiashara binafsi. Hata hivyo, ili kuimarisha bei ya mahindi, Serikali hutoa fedha kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).

 

39.        Mheshimiwa Spika, jana tarehe 9 Septemba 2021, Bunge lako tukufu lilipokea hoja binafsi kutoka kwa Mheshimiwa Justin Nyamoga, Mbunge wa Kilolo na kuungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge. Hoja hiyo, ililenga kuishauri Serikali kuingilia kati soko la mahindi ili kunusuru wakulima wa zao hilo.

 

40.        Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa shilingi bilioni 15 kwa ajili kuwezesha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mahindi maeneo mbalimbali nchini. Pia, Serikali ilitoa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko shilingi bilioni 10 kuongeza mtaji wa ununuzi wa mazao.

 

41.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kiasi hicho cha fedha ni kidogo ukilinganisha na uzalishaji wa mahindi uliopo. Hivyo, Serikali imesikia kilio cha wakulima kupitia Waheshimiwa Wabunge na kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa wakulima wa mahindi wanapata soko la mahindi waliyozalisha.

 

42.        Mheshimiwa Spika, tayari Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametoa shilingi bilioni 50 na ununuzi utaanza Jumatatu, tarehe 13 Septemba, 2021.  Hivyo, Wizara iendelee kutafuta masoko ya mahindi kwa kukamilisha mikataba mipya ya ununuzi wa mahindi na nchi za Sudan ya Kusini, DRC na Zimbabwe.

 

43.        Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeruhusu wafanyabiashara kutafuta masoko ya nje ya nchi ambapo vibali vya usafirishaji hutolewa kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Aidha, uuzaji wa chakula utafanywa kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na hifadhi ya kutosha ya chakula. Niendelee kusisitiza Wizara kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuongeza thamani ya mazao yetu ikiwemo mazao ya nafaka badala ya kuyauza nje yakiwa hayajaongezwa thamani.

 

44.        Mheshimiwa Spika, naiagiza Wizara ya Kilimo kuisimamia kwa karibu NFRA na CPB ili zinunue mahindi ya wakulima pekee, tena watoke ndani ya nchi. Aidha, ongezeni vituo vya kununulia mahindi hadi wilayani na kwenye miji midogo.

 

45.        Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Serikali inafuatilia mwenendo wa upatikanaji wa mbolea ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wingi na bei nafuu. Lengo la Serikali ni kuwezesha wakulima kumudu gharama za mbolea.

 

UJENZI WA MJI WA SERIKALI

46.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi wa Mji wa Serikali, mradi ambao unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa. Itakumbukwa kuwa katika awamu ya kwanza, Wizara 23 zilijenga ofisi zake na kuhamishia watumishi wapatao 18,300 jijini Dodoma. Aidha, ujenzi wa majengo ya kudumu ya wizara 23 na taasisi zake utaanza tarehe 30 Septemba, 2021. Ujenzi huo, utahusisha ipasavyo kampuni za ujenzi za umma na binafsi.

 

47.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia shilingi bilioni 300 zitumike katika awamu ya pili ya ujenzi huo. Kadhalika, shilingi bilioni 300 nyingine zitatolewa kadri ujenzi unavyoendelea. Hivi sasa, ujenzi wa miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, majisafi na majitaka, umeme, gesi, mifumo ya TEHAMA, huduma za zimamoto na upandaji miti unaendelea vizuri na kasi kubwa.

 

TAHADHARI DHIDI YA UVIKO-19

48.        Mheshimiwa Spika, Tanzania na dunia kwa ujumla bado imeendelea kupambana na ugonjwa wa virusi vya korona maarufu kama UVIKO-19. Janga limesababisha baadhi ya ndugu zetu kupoteza maisha na wengine kuendelea kuugua. Hivyo basi, hatuna budi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19.

 

49.        Mheshimiwa Spika, ninawasihi Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote, tufuate maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na pale mtu anapoona dalili ambazo hazielewi, awahi kwenye kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu ili afanyiwe uchunguzi na kupatiwa matibabu.

 

50.        Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kukabiliana na UVIKO-19, tarehe 28 Julai, 2021 Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo. Hivi sasa, chanjo hiyo inapatikana maeneo yote nchini katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma ya afya wilayani na mikoani.

 

51.        Mheshimiwa Spika, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote kuwa chanjo hii ni salama na haina madhara yoyote. Chanjo hiyo ambayo imethibitishwa na watalaamu na maabara zetu, ni hiyari lakini ni muhimu. Hivyo, niwaombe twendeni tukachanje ili kukabiliana na janga hili.

 

MATUMIZI YA MITANDAO

52.        Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumejitokea tabia ya baadhi ya watu kutumia vibaya haki ya uhuru wa mawazo na mifumo mbalimbali ya mawasiliano. Matumizi mabaya ya mitandao yamesababisha kusambazwa kwa taarifa za upotoshaji, kashfa, kutisha, na wakati mwingine kudhalilisha watu, kikundi au viongozi.

 

53.        Mheshimiwa Spika, katika kulinda na kutunza usalama, amani, maadili, umoja na mshikamano wa nchi ninawaagiza Mawaziri wa Mambo ya Ndani na mwenzake wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano watumie sheria, kanuni na taratibu zilizopo kuhakikisha vitendo na mienendo hiyo inadhibitiwa nchini.

 

MICHEZO

54.        Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba kumekuwepo na mwamko mkubwa wa masuala ya sanaa, burudani na michezo nchini. Hivi sasa, michezo imekuwa chanzo kikubwa cha biashara, utalii, kuimarisha afya na ajira kwa vijana wetu. Kwa kuzingatia hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kukuza michezo nchini. Hatua hizo zinahusisha kuundwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo na kurejesha mashindano ya UMITASHUMTA, UMISSETA na SHIMIWI.

 

55.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo nchini na kukubali kudhamini mashindano ya wanawake ya CECAFA ili kutoa motisha kwa wanawake kushiriki zaidi katika michezo. Mashindano hayo, yatajulikana kama Samia Cup sambamba na Kagame Cup kwa upande wa wanaume.

 

56.        Mheshimiwa Spika, Mfuko huo, utasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuziandaa vyema timu zetu za Taifa za michezo mbalimbali na kuziwezesha kushiriki kwa tija katika mashindano na michezo ya kimataifa. Pia, utatumika kuimarisha miundombinu ya michezo na upatikanaji wa vifaa vya michezo, kuendeleza na kuwezesha shule na vituo vya umahiri wa michezo, kuendesha programu za mafunzo ili kupata wataalaamu wa kutosha, kuwezesha programu za michezo kwa jamii na mashindano ya kitaifa na kimataifa.

 

57.        Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, michezo ni biashara na imekuwa chanzo muhimu cha ajira hususan kwa vijana. Aidha, ibara ya 243 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 inaielekeza Serikali kuanzisha mfumo thabiti wa michezo ya kulipwa ili kulinda na kuendeleza vipaji vilivyopo kwa manufaa ya Taifa letu na vijana kujipatia ajira kwa kutumia vipaji vyao. Tayari, Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imefanyiwa mabadiliko na kuruhusu michezo ya kulipwa na baadhi ya timu zetu zimeshaingia kwenye mfumo huo.

 

58.        Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa sheria hiyo, hivi karibuni, tumeshuhudia watalaamu wa michezo na wachezaji kutoka katika mataifa makubwa yaliyoendelea kimichezo wakija nchini kutafuta ajira kupitia michezo. Vilevile, tumeshuhudia uwekezaji mkubwa kwenye vilabu vyetu vikubwa nchini hususan Azam, Simba na Yanga na kuvifanya viendeshwe kibiashara.

 

59.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kwanza kuupongeza uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Wallace Karia kwa usimamizi mzuri wa soka nchini. Pili, nawapongeza sana wawekezaji na watendaji wa vilabu vya Azam, Simba na Yanga kwa uwekezaji mkubwa na usimamizi mzuri wa vilabu hivyo kwenye soka letu ambao umeanza kuzaa matunda.

 

60.        Mheshimiwa Spika, ninataka niwahakikishie wadau na wapenzi wa michezo kuwa Serikali itaendelea kuimarisha na kuvutia uwekezaji mkubwa katika tasnia ya michezo. Lengo ni kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wetu kimichezo ili waweze kushindana katika masoko ya michezo ya ndani na nje ya nchi, na hivyo kuimarisha ajira, mapato yatokanayo na shughuli za michezo pamoja na mchango wa sekta ya michezo katika pato la Taifa.

 

61.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuipongeza timu yetu ya Taifa ya Mpira wa Miguu (Taifa Stars) kufuatia ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Madagascar na hivyo kuongoza KUNDI J katika hatua ya pili ya kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar. Vilevile, tunaitakia kila la heri timu yetu ya wanawake ya kriketi inayoshiriki mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia la mchezo huo nchini Botswana na timu yetu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) itakayoshiriki mashindano ya COSAFA nchini Afrika Kusini kuanzia tarehe 28 Septemba, 2021 pamoja na kuitakia mafanikio timu yetu ya mchezo wa wavu inayoendelea kushiriki mashindano ya Afrika ya mchezo huo nchini Rwanda. Ninavitakia kila la heri pia vilabu vyetu vya Azam, Biashara United, Simba na Yanga katika uwakilishi wao kwenye michuano ya Shirikisho na Ligi ya Mabingwa ya Chama cha Soka barani Afrika (CAF).

 

62.        Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia kukipongeza kituo cha matangazo cha Azam (Azam Media) hususan upande wa matangazo ya runinga kwa kuuibua na kuutangaza vyema mchezo wa masumbwi nchini. Juhudi hizo za Azam Media wakishirikiana na wadau wengine zimewezesha wanamasumbwi wetu kutumia vizuri fursa hiyo kukuza vipaji vyao.

 

63.        Mheshimiwa Spika, niwapongeze mabondia wetu Twaha Kiduku kwa kumtwanga Dulla Mbabe katika pambano lililovuta hisia za Watanzania wengi. Vilevile, nimpongeze bondia Hassan Mwakinyo kwa kumdunda mpinzani wake Mnamibia Julius Indongo kwa TKO na kutetea mkanda wake wa Chama cha Ngumi Afrika (ABU). Wanamasumbwi wetu wameendelea kuifanya Tanzania itambulike zaidi ulimwenguni. Sasa tunasubiri pambano la watani Mwakinyo dhidi ya Kiduku.

 

HITIMISHO

64.        Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kumshukuru Katibu wa Bunge na watendaji wa ofisi ya Bunge kwa kazi kubwa ya kuratibu vikao vya mkutano huu. Aidha, niwashukuru watendaji wa Serikali kwa kufanikisha shughuli zilizopangwa na Bunge lako tukufu kwa weledi na ufanisi mkubwa.

 

65.        Mheshimiwa Spika, kipekee, niwashukuru wanahabari kwa kufikisha habari kuhusu mkutano huu kwa wananchi. Nivishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma wanazozitoa kwa washiriki wa Bunge hili bila kuwasahau madereva waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa Bungeni.

 

66.        Mheshimiwa Spika, natambua kuwa baada ya mkutano huu Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakuwa wakirejea majimboni kwao kuendelea na shughuli za kuwahudumia wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaeleza mambo yaliyojiri hapa Bungeni. Kwa hiyo, niwatakie safari njema na niwaombe kuwa mkawaeleze wananchi pia kuhusu matarajio yetu kwao na kuwasihi waendelee kutuunga mkono kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

 

67.        Mheshimiwa Spika, tarehe 19 Oktoba 2021, ikitegemewa na mwandamo wa mwezi, ndugu zetu Waislamu wataadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam. Hivyo, nitumie nafasi hii kuwatakia kila la heri katika maandalizi na hatimaye maadhimisho ya shughuli hiyo ya maulid ya kuadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam.

 

68.        Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 2 Novemba, 2021 siku ya Jumanne, saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu jijini Dodoma.

 

69.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 

 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news