Tanzania yavunja ukimya sakata la magari ya mizigo kuzuiliwa Malawi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema inafuatilia kwa karibu kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi taarifa kuhusu magari ya mizigo ya wasafirishaji wa Tanzania kuzuiliwa nchini humo.

Taarifa za awali kuhusu tukio hilo zinaeleza kuwa, tukio hilo limesababishwa na mgomo wa umoja wa madereva wa malori ya usafirishaji mizigo na mafuta nchini Malawi.

Umoja huo unaishinikiza Serikali ya nchi yao (Malawi) kuwasaidia madereva kuongezwa mishahara, kupunguziwa kiwango cha fedha za kuhuisha Hati za kusafiria na mahitaji yao mengine.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, baada ya umoja huo kuona ombi lao halijatekelezwa, walianzisha mgomo na kuhakikisha hakuna magari ya mizigo yanayotembea.

Hivyo, mkasa huo ukawakumba madereva wa Tanzania ambapo inakadiriwa takribani malori 60 ya Tanzania yamekwama nchini Malawi kutokana na mgomo huo.

Taarifa za Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, zinaeleza kuwa mgomo huo ulianza tarehe 28 Septembaa, 2021 jambo lililosababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara hususan katika maeneo ya kuingilia nchini humo ya Dedza, Mchinji na Karonga ili kuzuia magari yanayoingia Malawi au kupita nchini humo kwenda Afrika Kusini, Msumbiji na Zimbabwe.
Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mheshimiwa Benedicto Mashiba (katikati)akiwa katika picha ya pamoja na madereva walioegesha magari eneo la Kanengo-Lilongwe. (Na Mpigapicha Maalum).

Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi umewatembelea na kuzungumza na madereva katika baadhi ya maeneo waliyokwama ikiwemo eneo la Kanengo mjini Lilongwe na kwamba madereva hao wako salama pamoja na mali zao.

Baada ya jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi kufuatilia suala hilo, kwa sasa malori yameruhusiwa kuendelea na safari na kwamba jitihada za kuwasiliana na mamlaka za Malawi zinaendelea ili kuhakikisha madereva wa Tanzania wanakuwa salama wakati wakiendelea na safari kurejea Tanzania.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imemuelekeza Balozi wa Tanzania nchini Malawi Mhe. Benedicto Mashiba kukutana na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Malawi haraka iwezekanvyo ili kuona namna bora ya kutatua changamoto za usafirishaji zinazojitokeza.

Aidha, Wizara inawashauri madereva kutoa taarifa rasmi Ubalozini ili kupata msaada unaohitajika badala ya kutumia mitandao ya kijamii jambo linalozua taharuki kubwa.

Post a Comment

0 Comments