Viongozi wa dini Lushoto waongoza zoezi la chanjo

Na Yusuph Mussa, Lushoto

WACHUNGAJI wa makanisa mbalimbali Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wameongoza zoezi la uchanjaji lililofanyika Kijiji cha Migambo, Kata ya Migambo kwa wao wenyewe kuchanja chanjo ya UVIKO 19, huku Mkuu wa Wilaya ya Lushoto akishuhudia zoezi hilo.
Bi. Leylat Awadh wa Kijiji cha Kwefingo, Kata ya Migambo akipata chanjo ya UVIKO -19 kutoka kwa Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Theodora Tesha. (Picha na Yusuph Mussa).

Walioongoza zoezi hilo ni Mchungaji Vicent Maduda wa Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania (FPCT) Kata ya Migambo na Mchungaji Joshua Kipingu wa Kanisa Baptist Church of Tanzania kutoka Dindira, Kata ya Kwai.

Zoezi hilo la uchanjaji ambalo linafanyika pamoja na mikutano ya Mkuu wa Wilaya, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi, lilifanyika Kijiji cha Migambo Septemba 28, 2021, ambapo wananchi wamekuwa na muitikio mkubwa katika kuchanja chanjo hiyo, huku baadhi ya watu waliochanja chanjo hiyo wakipongeza hatua ya Serikali kupeleka chanjo ya UVIKO 19 kwenye kila zahanati, kituo cha afya na hospitali.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro (kushoto aliyesimama) akishuhudia Mchungaji Vicent Maduda wa Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania (FPCT) Kata ya Migambo akipata chanjo ya UVIKO 19 kutoka kwa Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Veronica Shehiza. Kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Lushoto Ramadhan Mahanyu. (Picha na Yusuph Mussa).

Mmoja wa wazee maarufu katika Kata ya Migambo ambaye pia alikuwa Diwani wa Kata hiyo Paul Twakyondo alisema uchanjaji wa Awamu ya Kwanza ulifanya wananchi kufuata chanjo mbali, ambapo yeye alikwenda kuchanja kwenye uzinduzi alioufanya Mkuu wa Wilaya.
Wananchi wa Kata ya Migambo wakisubiri vyeti vyao kutoka kwa Mratibu wa Chanjo katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Zawadi Mweta. (Picha na Yusuph Mussa).

Twakyondo alisema kwa sasa Serikali imepeleka chanjo hadi ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hospitali zote, hivyo wananchi wajitokeze sababu ni jambo muhimu kuchanja.

Naye Shekilindi aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo hiyo kwani itasaidia kuimarisha kinga ya mwili, ambapo hata mtu akiambukizwa hawezi kupata madhara makubwa.

Mkuu wa Wilaya Lazaro, alisema kuumwa UVIKO 19 ni hatari sababu inaweza kukuacha masikini ukaweza kuuza mashamba, nyumba ama vitu vyako vya thamani ili uweze kupata matibabu.
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro (katikati) akishuhudia Mchungaji Joshua Kipingu wa Kanisa la Baptist Church of Tanzania Dindira, Kata ya Kwai akipata chanjo ya UVIKO 19 kutoka kwa Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Veronica Shehiza. Kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Lushoto Ramadhan Mahanyu na kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto Shaaban Shekilindi 'Bosnia'. (Picha na Yusuph Mussa).

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Lucy Maliyao alisema kwa Septemba 28, 2021 waliochanja kwa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto ni 130, ambapo kati yao, 44 walichanja kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge na Mkuu wa Wilaya.

Post a Comment

0 Comments