Wakuu wa mikoa, wilaya mtegoni kuhusu Machinga nchini

NA GODFREY NNKO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa kuchukua hatua zinazostahili katika zoezi la kuwapanga Wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) nchi nzima bila kuleta vurugu, fujo na uonevu.
Mheshimiwa Rais Samia amesema, hali ya Machinga kuonekana kila mahali hasa mbele ya milango ya maduka kunasababisha Serikali kushindwa kukusanya mapato.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Septemba 13,2021 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma wakati akiwaapisha Mawaziri Watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Amesema, ni kutokana na ukweli kuwa wenye maduka ambao ndio walipa kodi hushindwa kufanya biashara zao.

Mheshimiwa Rais amesema kuwa, anajua kwamba Serikali imetoa fursa kubwa kwa Machinga kufanya shughuli zao.

"Watu hawa wamekuwa wakifanya kazi katika maeneo tofauti tofauti. Wakuu wa mikoa wanawapanga...wakuu wa wilaya wanawapanga. Lakini wameenea kila mahali mpaka kwenye maduka, wao wanaziba maduka hayauzi wao wanauza.

"Baadhi ya wenye maduka wanatoa bidhaa ndani na kuwapatia machinga kuuza kwa sababu watu hawaingii ndani. Tendo hili linatukosesha kodi kwa sababu mwenye duka analipa kodi na machinga halipi.

"Wito wangu kwa wakuu wa mikoa mkawapange vyema. Sitaki kuona yale ninayoyaona kwenye TV.

"Niwaombe Wakuu wa Mikoa kupitia televisheni kuchukua hatua zinazostahili bila kuleta vurugu fujo na uonevu. Wito wangu kwa machinga wajitahidi kufuata sheria na kanuni zilizopo,"amesema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia amewataka viongozi kufanya kazi kwa vitendo zaidi badala ya kutoa maneno makali akisema Serikali itaendeshwa kwa matendo makali siyo maneno makali.

"Kipindi cha miezi sita nilikuwa najifunza, Nilikuwa Makamu wa Rais, nilikuwa na nyinyi lakini sikuwa na fursa ya ndani ya kujifunza utendaji wa ndani ya Wizara mbalimbali. Nimekuwa nikijifunza na nimeona sasa vipi nakwenda na nyie.

Katika uongozi kuna mbinu nyingi. Nami nimejichagulia mbinu yangu. Nataka niwaambie kuwa tunakoendelea huko Serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na siyo maneno makali. Ninaposema matendo makali wala siyo kupigana mijeledi, ni kwenda kwa wananchi kutoa huduma inayotakiwa, kila mtu kufanya wajibu wake,"amesema Rais Samia.

"Msinitegemee kwa maumbile yangu haya, pengine na malezi yangu kukaa hapa nianze kufoka weyee..wawawaaaaa! Nahisi siyo heshima, na kwa sababu nafanya kazi na watu wazima, wanaojua jema na baya ni lipi.

"Kwa hiyo ni imani yangu kwamba tunapozungumza tunaelewana na kila mtu anajua afanye nini kwenye wajibu wake. Kwa hiyo msitegemee nianze kufoka ovyo ovyo, kufokea watu wazima wenzangu,nitafoka kwa kalamu,"amesema Rais Samia Suluhu Hassan.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news