WATELEKEZA OFISI YA KIJIJI MIAKA MINNE,WAKIMBILIA MGODINI

Na Robert Kalokola, Diramakini Blog

Wananchi wa Kijiji cha Busolwa B Kata ya Nyarugusu Wilaya ya Geita wamelalamikia viongozi wa serikali ya kijiji hicho kutelekeza na kufunga ofisi ya kijiji zaidi ya miaka minn e na kwenda kufanyia kazi katika majengo yasiyo na hadhi katika eneo la machimbo ya dhahabu maarufu kama machimbo ya Stamico.
Ofisi ya Kijiji cha Busolwa B ambayo Mwenyekiti na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho wameitelekeza.

Katika mazungumzo na DIRAMAKINI Blog, wananchi hao wanasema, wanashindwa kupata huduma kwa wakati kutokana na umbali uliopo wa zaidi ya kilomita tatu hadi ofisi ilipo kwa sasa ambayo Mwenyekiti wa Kijiji ,Afisa Mtendaji wa Kijiji pamoja na Mwenyekiti wa kitongoji wamehamishia shughuli za ofisi mgodini.

Uwepo wa viongozi hao mgodini,unadaiwa kuchochea vurugu mgodini,na kusababisha viongozi hao kufunguliwa kesi mahakamani kwa madai ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu na kusababisha vurugu katika mgodi huo.

Shauri hilo limeamuliwa mahakamani na kuamuru viongozi hao waondoke mgodini na kurudi kwenye ofisi ya Busolwa B ndani ya siku 30,lakini hadi sasa ni zaidi ya siku 120,amri hiyo haijatekelezwa na viongozi hao.
Ameongeza kuwa, sababu nyingine ya kuhamia mgodini ni kutoka na eneo hilo la machimbo kuwepo idadi kubwa ya watu ambao wanahitaji kuhudumiwa na ofisi ya kijiji hicho.

Licha ya ofisi iliyojengwa na Mwekezaji kuonekana ina hadhi kuliko jengo la mgodini wananchi wamedai kushangazwa kuona mwenyekiti na afisa mtendaji wa kijiji hicho kuhamisha ofisi na kwenda kufanyia kazi katika machimbo hayo.

Mwenyekiti wa kijiji na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho hawakuwa tayari kuongelea suala hili,lakini mmoja wa wajumbe wa serikali ya kijiji ameeleza sababu zilizowafanya kukaidi agizo la mahakama.

Anna Robert ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Busolwa B amesema kuwa,wananchi kwa kushirikiana na mwekezaji walijenga ofisi ya kijiji na kwamba ofisi hiyo haiwezi kutumika kwa sababu haijakamilika, hivyo walilazimika kuhamia mgodini.

Josia Nyalanga na na Elina Richard wamesema kuwa, si uongozi wa kijiji pekee waliokimbia hata mwenyekiti wa kitongoji cha Nyasale naye amekimbilia mgodini huko,hivyo ni ngumu kuwapata katika eneo la ofisi hiyo.

Neema Jerald mkazi wa Kitongoji cha Nyasale amesema kuwa, wananchi wanapohitaji huduma kutoka kwa mwenyekiti wao wa kitongoji wanashindwa kupata huduma kwa sababu muda mwingi anakuwa kwenye vilabu vya pombe inabidi kuanza kumsaka huko.

Ng’oni Sanagu ambaye ni Mwenyekiti Kitongoji cha Nyasale amesema kuwa, yeye hajahamisha ofisi bali mwenyekiti wa kitongoji hana ofisi maalum, hivyo analazimika kutoa huduma sehemu yoyote ile anapokuwa yeye.

Viongozi wa mgodi wa Stamico wamesema, wao ndiyo wenye mamlaka kwa mujibu wa sheria kukusanya kodi za serikali kwa niaba ya Tume ya Madini na Halmashauri ya wilaya pamoja na kusuluhusisha migogoro yote inayohusu shughuli za uchimbaji.
George Kwacha Meneja na Msimamizi wa Mgodi wa Stamico. ( Picha na Robert Kalokola).

George Kwacha ambaye ni msimamizi wa mgodi wa Stamico amesema kuwa, haijawahi kutokea tatizo lolote kuhusiana na shughuliza za uchimbaji uongozi wa mgodi huo ukashindwa kusuluhishwa na kutatua matatizo hayo.

Ameongeza kuwa, uongozi huo wa mgodi unaangalia kazi zote za mgodi ikiwemo usalama katika mgodi katika mashimo ,usafi wa mazingira,mgao wa mawe pamoja na kukusanya mapato yote ya serikali.

Ameongeza kuwa,hakuna matatizo yoyote yanayohusiana na uchimbaji yanaruhusiwa kusuluhishwa katika ofisi ya serikali ya kiji isipokuwa yanatatuliwa na uongoz wa mgodi kwa kushirikiana na ofisi ya madini ya mkoa.
Paul Wanga Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita akizumgumzia sakata la viongozi wa serikali ya kijiji cha Busolwa B kukimbia Ofisi. (Picha na Robert Kalokola).

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Paulo Wanga amesema, suala hilo amelipokea kwa mara ya kwanza na kuahidi kulifuatilia ili kujua undani wake na kwamba endapo akikuta kuna ukweli basi atahakikisha analitatua ndani ya siku kumi na nne na viongozi hao wa kijiji wanarudi kwenye ofisi hizo kuhudumia wananchi.

Post a Comment

0 Comments