Waziri Mhagama:TUGHE ni chama bora cha kuigwa nchini

Na Rotary Haule,Dodoma

WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera,Bunge Taratibu,Ajira,Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama amekimwagia sifa kemkem Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kwa kutaka watembee kifua mbele kwa kuwa ndio chama pekee kinachotekeleza majukumu yake kikatiba.

Aidha,Mhagama amesema kutokana na hali hiyo ameahidi kutoa mafunzo maalum kwa viongozi wapya wa TUGHE watakaochaguliwa kukiendesha chama hicho kwa muda wa miaka mitano ijayo.
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu ,Sera,Bunge, Taratibu, Ajira na Walemavu Jenister Mhagama wa nne kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TUGHE Taifa mara baada ya kufungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho leo Septemba 29 Mjini Dodoma. (Picha na Rotary Haule).

Mhagama ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa TUGHE uliofanyika jijini Dodoma ukiwa umeshirikisha wajumbe zaidi ya 234 kutoka mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Amesema kuwa,TUGHE ni mfano wa kuigwa na vyama vingine kwa kuwa kazi wanayofanya ni kubwa na imekuwa na mafanikio makubwa kwakuwa inaunganisha wafanyakazi na Serikali .

Mhagama ameongeza kuwa, hata TUCTA imekuwa na imani kubwa na TUGHE kwa kuwa chama hicho kimesheheni kila kitu, kina hazina ,hekima,busara na weledi mkubwa huku akisema lazima TUGHE ilindwe kwa nguvu zote.

''TUGHE imekuwa ikifanya vizuri sana ndio maana hata Rais alipokuja kwa mara ya kwanza katika maadhimisho ya Mei Mosi alikuta TUGHE imeandaa vizuri maadhimisho hayo kiasi ambacho kilimvutia Rais,"amesema Mhagama.

Mhagama,amesema ukiachia mbali Rais, lakini hata viongozi wengine wa juu akiwemo Makamu wa Rais,Waziri Mkuu na yeye binafsi wamekuwa wakikiheshimu chama hicho na mara zote wapo tayari kushirikiana na viongozi wake katika kufanya mazungumzo yanayolenga maslahi ya wafanyakazi.

Amesema kuwa, TUGHE kimekuwa kikifanya kazi zake kwa mujibu wa katiba na hata mkutano mkuu wa uchaguzi upo kikatiba na kufanya kuwa chama cha kwanza nchini kufuata katiba jambo ambalo limekuwa likiungwa mkono na Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Mhagama amemuagiza msajili wa vyama vya wafanyakazi awape salamu vyama vingine ambavyo havitaki kufanya uchaguzi kikatiba na kwamba wakishindwe kufanya hivyo sheria itachukua mkondo.

Ukiachilia sifa hizo, lakini pia Mhagama ,amesema kuna kila sababu ya kukilinda chama hicho kwa nguvu zote na kamwe wasikubali aje mtu kuwavuruga huku akitaka wasonge mbele kwa faida ya chama,wanachama na Taifa.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Septemba 29 na Septemba 30, mwaka huu Mhagama amewataka wajumbe kuhakikisha wanachagua viongozi wazuri watakaozidi kukiimarisha chama badala ya kuchagua watu wenye maslahi yao binafsi.

"TUGHE ipo mstari wa mbele kupambana na COVID -19,inatoa mchango mkubwa kwa Serikali kufikia mapato ya kati ,ndio maana Serikali inaendelea kujipanga kuona namna ya kuongeza jitihada za kushirikiana na TUGHE katika mapambano ya kuijenga nchini,"amesema Mhagama.

Aidha,amewaomba wanachama wa TUGHE na viongozi wake kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ili apate moyo wa kusonga mbele zaidi katika kutekeleza yale anayokusudia katika nchi.

Amesema kuwa,Rais Samia Suluhu Hassan mara alipoingia madarakani alipokea kero ya mabadiliko ya sheria ya bima ya afya kuhusu umri wa wategemezi kutoka miaka 18 mpaka 21 lakini jambo hilo limekamilika.

Amesema kuwa,Rais pia alipokea kilio cha wafanyakazi juu ya tozo ya mikopo ya asilimia 6, lakini aliagiza ifutwe na kupunguza kodi kwa wafanyakazi kutoka asilimia 9 mpaka 8 jambo ambalo limeleta unafuu kwa wafanyakazi nchini na kusema jitihada hizo za Rais ni vyema zikaungwa mkono.

Hata hivyo ,pamoja na mambo mengine Mhagama amewataka waajiri waanze kujitathimini ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kuwepo kwa vyama vya wafanyakazi pamoja na mabaraza ya wafanyakazi kwa kuwa ni sehemu ya kuwaunganisha wafanyakazi na Serikali.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda,amesema kuwa ndani ya miaka mitano chama kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza wanachama na kufikia 23,008,kuongeza mapato na kukuza demokrasia ndani ya chama.

Mkunda,ametaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kununua viwanja 29 sehemu mbalimbali vitakavyosaidia kujenga vitega uchumi, kuboresha vitendeakazi,na kufanya maamuzi ya asilimia 20 ya mapato ibaki katika tawi husika.

Hata hivyo, mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Archie Mntambo amesema kuwa, chama kina malengo mengi na hata mafanikio yaliyopatikana yametokana na ushirikiano wake na baraza lake.

Mntambo,amesema kuwa, TUGHE inabeba taswira ya Serikali na kwamba wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa ajili ya faida ya chama,wanachama na Taifa kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news