Waziri Simbachawene atoa maagizo kwa Jeshi la Magereza

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amelitaka Jeshi la Magereza nchini kuacha kuwafunga wafungwa kikoloni kwa kuwatesa na kuwanyima haki zao za msingi na badala yake kutumia wafungwa hao kama nguvu kazi ya kuleta mafanikio magerezani.
Amesema, jeshi ni sehemu ya kujifunza hivyo watumie sehemu hiyo kuwarekebisha,kuwafundisha kuwa raia wema hata wanaporejea katika jamii waonekane jeshi limefanya kazi nzuri.

Simbachawene amesema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa maafisa waandamizi wa Jeshi la Magereza wenye lengo la kujadili changamoto wanazokumbana nazo, na tathimini ya shughuli zinazofanywa na Jeshi la Magereza.

Amesema,  wafungwa wengi wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi wanapokuwa gerezani ikiwemo kulala,kubadilisha nguo na kula kwa wakati na kusahau kuwa mfungwa ndio rasilimali mtu katika gereza.

Amesema kuwa, wafungwa walioko kwenye Magereza wanapaswa kupewa haki zao za msingi kama kuwapa kwenda kwenye nyumba za ibada kwa ambao wanakwenda msikitini waende msikitini na wa kanisani waende kanisani.

"Ni ukweli usiopingika jeshi hili mmejitahidi sana endeleni kuwa wabunifu wa miradi mbalimbali pia tumieni hawa wafungwa kama rasilimali watu,lindeni mafanikio haya ili yalete matunda," amesema Simbachawene.

Sambamba na hayo amesema kuwa, mbali na miradi hiyo zilizopo askari wanapaswa kutengeneza fedha kupitia miradi hiyo iliyopo ambayo ni mashamba wayatumie kwa kulima mazao mbalimbali.

Kwa upande wake Kamishina Jenerali wa Magereza, Suleiman Mzee amewataka maafisa hao kutumia mkutano huo kujadili na kuleta maendeleo katika maeneo wanayo simamia kuimarisha sekta ya kilimo.
Amesema kuwa, mbali na kuimarisha Sekta ya Kilimo wameweka mazingira ya kujitegemea kwa kufungua miradi mingi ya ubunifu ikiwemo ujenzi wa nyumba za makazi ya maafisa na askari,ujenzi wa makao makuu ya jeshi, ununuzi wa vitendea kazi, hali iliyopelekea kuondokana na utegemezi.

Amesema kuwa, mwaka jana kulifanyika mkutano mkuu ambao uliweka maazimio ya kujenga makao Makuu ya Magereza ambapo maazimio hayo tayari wameyafanyia kazi.

"Tumefanikiwa kutembea maeneo yote nchini kasoro Kisiwa cha Mafia na Mkoa wa Iringa kwa kuwa na utekelezaji hasa katika kujenga mabweni ya wafungwa na miradi mingi inayoendelea nchini,magari,mashine,mikopo,kampuni ya ulinzi pamoja na viwanda,"amesema.

Ameendelea kusema kuwa, jeshi hilo la Magereza limefanikiwa katika maeneo mbalimbali ambapo alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za wafungwa ukarabati wa baadhi ya Magereza na ujenzi wa kiwanda cha mikate kilichopo Msalato na mafanikio mengine.

Ameendelea kusema kuwa, mabadiliko ya uongozi wa Magereza yaliyofanyika hapo nyuma yamefanya jeshi hilo kuwa na miradi ambayo umewafanya kujitegemea wenyewe bila kutegemea Serikali.
Hata hivyo, Waziri huyo ameweka jiwe la msingi katika sehemu ya kutengenezea mikate (Bakery), kisima cha maji na nyumba 34 za maafisa askari wa makao makuu ambapo maadhimisho hayo yamebebwa na kauli mbiu isemayo '' Fikra mpya, mtazamo mpya kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea".

Post a Comment

0 Comments