Ulinzi shirikishi ni mzuri, upeni kipaumbele-Shila

Na Anneth Kagenda, Diramakini Blog

Watanzania katika maeneo mbalimbali na hasa viongozi wa Serikali za mitaa inayolizunguka eneo la Viwanja vya Ndege wameaswa kuendelea katika kujiimarisha na Ulinzi Shirikishi kwenye mitaa yao jambo ambalo litasaidia kupunguza uhalifu kwa kiasi kikubwa na kutunza mazingira.
Wito huo umetolewa Dar es Salaam na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Jeremia N Shila ambaye ni Kamanda wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege Tanzania, wakati akikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya Ulinzi Shirikishi katika Mtaa wa Sigara uliopo Kata ya Yombo Vituka katika Jimbo la Temeke.

Kamanda amesema, suala la ulinzi shirikishi ni la kila mtu na kwamba kwa wale waliopewa ridhaa wanatakiwa kuthaminiwa zaidi na ndio maana wameona upo umuhimu wa kukabidhi vifaa hivyo ili vijana wa ulinzi shirikishi waweze kufanya kazi zao kwa weledi zaidi.

"Nipende kusema ukweli kwamba lengo kuu lililotufanya tuone umuhimu wa kutoa vifaa hivi watu wa TAA pamoja na watu wa Viwanja vya Ndege ni kutokana na kwamba watu wa Sigara mna mchango mkubwa sana kwenye ulinzi shirikishi," amesema Kamanda Jeremia na kuongeza;

"Na hasa kwenye maeneo yetu haya yanayozunguka Viwanja hivi vya Ndege vya Mwalimu Julius Nyerere,hivyo niwaombe muendelee na ushirikiano huu huu na hata kwa ulinzi wa mazingira,".

Aidha, amewatoa wasiwasi uongozi wa Serikali hiyo na kuwaambia kuwa, jeshi hilo liko tayari kutoa elimu kwa vijana wa ulinzi shirikishi hivyo ni vyema mtaa huo ukajipanga na badaye kutoa taarifa ili jeshi hilo liweze kutoa mafunzo na mbinu elekezi kwa vijana ili weweze kujua jinsi ya kutumia dhana mbalimbali hasa nyakati za usiku wanapokuwa lindoni.

Mkuu wa Kitengo cha Mazingira kutoka TAA, Maxmilian Mahangila ameutaka pia uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Sigara kuendelea kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kutoacha madampo ya vyakula yakizagaa ovyo ili kuepuka ndege warukao pamoja na mbwa ambao badaye wanaweza kuingia kwenye viwanja vya ndege na kuleta madhara.

Amesema, pia wamekuwa wakishirikiana kwa ukaribu na uongozi wa serikali za mitaa pamoja na ulinzi shirikishi kwa mitaa yote mitatu inayowazunguka katika kuhakikisha ndege hai kama mbwa, kunguru na wengine hawasababishi hatari hasa kuingia kwenye uwanja wa ndege za abiria hivyo ni lazima kusiwepo na madampo ovyo maeneo mbalimbali mitaani, kwani ni hatari zaidi kuwepo madampo karibu na maeneo yanayozunguka uwanja.

"Niwaombe uongozi pamoja na watu wa Ulinzi Shirikishi kuendelea kushirikiana katika kutunza mazingira ili tuweze kuendelea kutunza ndege hai na wale warukao ili waendelee kuishi, lakini pia wasiharibu katika mazingira mengine yanayohusu ndege zinazobeba abiria," amesema Mahangila.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sigara, Philemon Gotta, aliomba viongozi hao kutembelea zahanati iliyopo kwenye mtaa wake ikiwa ni pamoja na kuwapa msaada wa vifaa mbalimbali pale tu watakapopata nafasi.

"Tunashukuru kwa msaada mliotupa, lakini niseme kwamba vifaa tulivyopewa havitoshi ni vichache hivyo mkijaliwa tena tunaomba mtutupie jicho kwa mara nyingine tena, pia tunaomba kuongezewa tochi,kwani kuna maeneo mengine ambayo kuna giza sana na wahalifu wamekuwa wakitumia mianya hiyo kufanya uhalifu," amesema Mwenyekiti Gotta.

Ameomba pia viwanja vya ndege kuwapa nafasi ya kwenda kutembelea uwanjani hapo ambapo Mahangila alisema suala la kutembelea uwanjani hapo halina shida na kwamba la zahanati na tochi aliyachukua na atayashughulikia.

Mwenyekiti alisema mtaa wake pamoja na Viwanja vya Ndege wanao ushirikiano mzuri na kwamba ulinzi umeimarishwa vizuri wako juu, na kwamba vifaa vilivyotolewa katika Serikali hiyo ya Mtaa ni pamoja na Virungu 15, Tochi 7, Jacket za mvua 15, Buti 12, Reflekta 10 na Filimbi 7.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news