World Vision yatumia Bilioni 2.3/- miradi ya maendeleo Mnyuzi AP wilayani Korogwe

Na Yusuph Mussa, Korogwe

SHIRIKA la World Vision Tanzania kupitia Kanda ya Mashariki, limeweza kutoa sh. bilioni 2,372,044,036 kwa mwaka 2019-2021 ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Mradi wa Mnyuzi (AP) uliopo kata za Kwagunga na Mnyuzi katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Basilla Mwanukuzi (kushoto) akifungua koki kama ishara ya kutaka kujua maji yanatoka. Ni mradi wa maji Kijiji cha Kwagunda uliojengwa na Shirika la World Vision kwa kushirikiana na RUWASA ambao walitoa wataalamu. Mradi umegharimu sh. milioni 236. (Picha na Yusuph Mussa).

Mradi huo wa Mnyuzi AP, unatekeleza shughuli za maendeleo ya jamii na ustawi wa watoto katika Kata ya Kwagunda na Mnyuzi katika vijiji 12, ambavyo ni Ubiri, Mng'aza, Mkokola, Magunga Cheki, Kwagunga, Gereza East, Mkwakwani, Kwamzindawa, Mnyuzi, Lusanga, Ngomeni na Shamba Kapori.

Hayo yamesemwa Septemba 11, 2021 na Mratibu wa Mradi wa Mnyuzi AP, Alice Mmbaga wakati anawasilisha kazi zilizofanywa na shirika hilo kwa kipindi hicho cha 2019-2021 kwenye kikao cha wadau wa maendeleo kikijumuisha viongozi wa jamii na vijiji kutoka kata husika, lakini pia wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kutoka idara husika, huku Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basilla Mwanukuzi akiwa mgeni rasmi.

"Mradi wa Mnyuzi unatekeleza shughuli zenye lengo la kuboresha maji na usafi wa mazingira, usalama wa chakula na lishe, afya, elimu pamoja na mambo mtambuka kama vile utetezi na utunzaji wa mazingira. Mradi umekuwa ukitoa mafunzo kwa jamii ili kuchangia mabadiliko endelevu ya kiuchumi kwa jamii.

"Uwezeshaji huo umejikita zaidi katika kuwezesha jamii kuwa na mtazamo chanya, ikiwa ni pamoja na kuisaidia jamii kutambua na kutumia rasilimali zilizopo katika maeneo yao kubadili hali yao ya kimaisha. Aidha kuanzia mwaka 2019, mradi kwa kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, uliwezesha ujenzi wa miundombinu na kuwezesha mafunzo mbalimbali,"amesema Mmbaga.
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa choo Shule ya Msingi Mseko iliyopo Kijiji cha Kwagunda, ambapo Shirika la World Vision linajenga matundu ya vyoo 16 kwa gharama ya sh. milioni 68. Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basilla Mwanukuzi (hayupo pichani), alifika kuangalia ujenzi wa choo hicho ikiwa ni ziara ya kukagua miradi inayogharamiwa na shirika hilo. (Picha na Yusuph Mussa).

Mmbaga alitaja sekta zilizopata fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi, ambapo maji, usafi, afya na lishe walipata sh. milioni 934,628,252 sawa na asilimia 39.40, kilimo na ufugaji sh. milioni 280,880,200 asilimia 11.84, elimu sh. milioni 556,994,196 asilimia 23.48, ufadhili wa mambo mtambuka sh. milioni 354,894,388 asilimia 14.96 na kazi zinazoendelea ni sh. milioni 244,647,000 asilimia 10.31, ambapo jumla ni sh. bilioni 2,372,044,036.

Mmbaga alisema Mradi wa Mnyuzi AP kwa kushirikiana na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Korogwe pamoja na Ofisi ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, wameunda jumla ya jumuiya tatu za watumia maji katika kata zote mbili za Kwagunda na Mnyuzi. Jumuiya hizo zenye wajumbe 80, wamewezeshwa juu ya usimamizi na majukumu ya jumuiya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basilla Mwanukuzi (katikati) alifika Shule ya Msingi Mseko iliyopo Kijiji cha Kwagunda kuangalia ujenzi wa maeneo ya kunawa mikono kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo, ambapo Shirika la World Vision limejenga kalo hizo mbili kwa gharama ya sh. milioni 16. (Picha na Yusuph Mussa).

Alisema wajumbe hao ndiyo waelimishaji kwa jamii juu ya umuhimu wa ukusanyaji wa fedha, utunzaji wa miundombinu na vyanzo vya maji, na sheria nyingine ndogondogo, ambapo mafunzo hayo yamegharimu sh. milioni 4,024,000.

"Katika kipindi cha mwaka 2019-2021, mradi umefanikisha kuchimba visima viwili na ujenzi wa miundombinu ya maji (tenki 4 zenye ujazo wa lita 50,000 na nyumba za pampu mbili), vyanzo vya maji mtiririko viwili, mitambo ya nishati ya ju miwili, pampu mbili, mtandao wa maji na vituo 49 vya kuchotea maji (vilula).

Ambapo vilula hivyo Kwagunda ni 14, Magunga Cheki 10, Mkokola 18 na Mng'aza saba. Na wamefanikisha ujenzi huo kwa usimamizi wa wataalamu wa RUWASA Wilaya ya Korogwe na Shirika la World Vision Tanzania. Kwa sasa zaidi ya wanajamii 9,000 wanapata maji safi kwa matumizi ya nyumbani. Na miradi hiyo imegharimu sh. milioni 835,454,252.
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Basilla Mwanukuzi (wa pili kushoto), alifika Shule ya Msingi Mseko katika Kijiji cha Kwagunda kukagua miradi inayogharamiwa na Shirika la World Vision, ambapo linajenga matundu ya vyoo 16 kwa gharama ya sh. milioni 68. (Picha na Yusuph Mussa).

"Pia, mradi umewezesha ujenzi wa vinawia mikono katika shule saba za Kwagunda, Fumbo, Kwamzindawa, Lwengera Estate, Mnyuzi, Mseko na Shule ya Sekondari Kwagunda. Nia ikiwa kuhamasisha usafi hususani kipindi hiki cha janga la UVIKO 19. Kwa kushirikiana na Afisa Afya Wilaya ya Korogwe, mradi umefaniksha kutoa elimu kwa wanajamii wa vijiji vyote 12 kupitia mikutano ya hadhara, na maofisa kutembelea katika kaya kwa uhamasishaji zaidi, ili kusisitiza jamii kutumia vyoo bora, na jumla ya sh. milioni 45,200,000 zimetumika,"amesema Mmbaga.

Meneja wa Shirika la World Vision Tanzania Kanda ya Mashariki Pudensiana Rwezaula alisema shirika hilo limejikita kuona wananchi wanapata maendeleo kwa kuboresha huduma za jamii na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja ikiwa ni katika kuwaondolea umasikini, huku akiomba ushirikiano kwa wadau wa maendeleo na Serikali ili kuweza kufanikisha hayo yote.
Nyumba ya Pampu ya Maji iliyopo Kijiji cha Mng'aza, Kata ya Kwagunda. Nyumba hiyo ni sehemu ya mradi wa maji uliojengwa na Shirika la World Vision kwa gharama ya sh. milioni 236. (Picha na Yusuph Mussa).

Mkuu wa Wilaya, Mwanukuzi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho aliwaomba World Vision kuendelea kutoa huduma kwenye kata za wilaya hiyo, kwani mahitaji ni mengi, huku akitoa mfano wa madarasa ya Shule ya Msingi Goha iliyopo Kata ya Mkumbara, ambapo alipofanya ziara kwenye shule hiyo, alikuta madarasa ni chakavu.

"Mahitaji kwa wananchi bado ni mengi, kwani pamoja na jitihada za Serikali kuweza kujenga miundombinu ya elimu, bado kuna shule nyingine zinahitaji msaada kama shule moja ya msingi (Goha) iliyopo Kata ya Mkumbara. Kwa kweli bado msaada wa World Vision unahitajika" alisema Mwanukuzi

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news