Jiji la Tanga laahidi kuzingatia uwazi kwa fedha zote

NA HADIJA BAGASHA

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imeahidi kutekeleza agizo la Serikali Kuu la uwazi katika kutoa taarifa za mapato na matumizi na kuweka hadharani mapokezi ya fedha yote kutoka Serikali Kuu kwa kipindi husika.
Akizungumza katika kikao cha Madiwani cha Halmashauri ya Jiji la Tanga kilichofanyika jijini hapa, Mkurugenzi wa Jiji, Spora Liana alisema agizo hilo lilitolewa miaka mingi iliyopita (tangu enzi za Utawala wa Awamu ya Tatu iliyoongozwa na aliyekuwa Rais hayati Benjamin Mkapa mwaka 1995).

Alisema, ni takwa la serikali kuona kwamba fedha zote zinazoingia na kutoka ni lazima zitolewe taarifa kupitia vyombo vya habari pamoja na kuzitangaza kupitia mbao za matangazo ili wananchi wazione na kusoma.

“Tukipokea fedha zozote ni lazima wananchi wote wazisome, hali kadhalika wananchi wote wawe na haki ya kufahamu fedha zilizopokelewa zinafanyia kazi gani. Kwa mfano, bweni au darasa linapojengwa, wananchi wanastahili kufahamu gharama na hata mapato yetu yanayokusanywa, yapaswa yafahamike pia,”amesema.

Kauli hiyo ya Mkurugenzi wa Jiji ilikuwa inaunga mkono nasaha za Mtahiki Meya, Abdrahaman Shiloo aliyesisitiza uwazi katika mapokezi na matumizi ya fedha ya serikali, iwe ya makusanyo ya ndani au kutoka serikali kuu.
Mkurugenzi huyo wa Jiji aliweka wazi mapokezi ya hivi karibuni ya fedha kutoka serikalini, akiweka wazi kwamba serikali kuu tayari imekwishaleta jumla ya sh. bilioni 1.244,900,276/027 kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Hata hivyo pamoja na majadiliano kuhusu miradi ya maendeleo, wajumbe pia walizungumzia kuhusu ukiukwaji wa masharti ya ujenzi uliofanywa na kiwanda cha Rhino kujenga hosteli kiwandani hapo kinyume na masharti ya ujenzi kwani eneo hilo ni kwa shughuli za viwanda tu (industrial area) na sio sehemu ya makazi, na hivyo kuagiza idara husika kufuatilia na kuchukua hatua stahiki ili kurekebisha mapungufu hayo.
Akichangia kuhusu utekelezaji miradi ya maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandila, aliipongeza uongozi wa jiji kwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa na hivyo kutaka mashirikiano ya karibu kati ya uongozi na wananchi kwa kuwashirikisha katika maamuzi yanayowahusu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news