DC Mgandilwa afichua yalipo madanguro Tanga, atoa maagizo

NA HADIJA BAGASHA

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Mgandilwa ameyataja maeneo yanayotumika kwa ajili ya biashara ya kuuza miili maarufu kama madanguro yanayotumiwa na dada poa, ambapo ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha biashara hiyo kwenye maeneo hayo inakoma mara moja.
Agizo hilo amelitoa kwenye kikao cha cha baraza la madiwani wa halamashauri ya jiji la Tanga.

Mgandilwa ameyataja maeneo hayo kuwa ni eneo la Sabasaba na barabara ya Uhuru na kusema kuwa wanaofanya biashara kwenye maeneo hayo watafute miji mingine.

"Kuna maeneo kwetu sisi bado kuna madanguro ambayo dada zetu wanajiuza, naomba nitumie hadhara hii kwa kuwa vyombo vya dola vipo hapa niwaombe tuanze kushughulika na hawa watu natamani tuone mji wetu unakuwa safi, hatutaki kuona hizi biashara za kujiuza jeshi la polisi wakati mkifanya operesheni zenu basi mshughulike na watu hawa,"alisistiza DC Mgandilwa.

Katika hatua nyingine Mgandilwa amesema, pamoja na hayo analipongeza jiji hilo kwa kuweza kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi na kutaka kuwalipa fidia wananchi ambao bado wana migogoro ya fidia zao lengo ni kuondokana na migogoro isiyokuwa na lazima.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji la Tanga, Abdulrahman Shiloo amewataka wakuu wa idara kuheshimu maamuzi yanayofanywa na baraza la madiwani ili kuepukana na migongano isiyokuwa ya lazima inayoweza kukwamisha jitihada za maendeleo kwenye jiji hilo.

"Nitoe angalizo kwa wakuu wetu wa idara na watumishi wote wa halmashauri wapatao 3000 waelewe kwamba kikao cha mwisho chenye maamuzi katika jiji hili ni baraza la madiwani, hivyo wasijaribu wala wasiwaze kujikweza kimadaraka hakikisheni sheria, kanuni taratibu na miongozo zinafuatwa ili tusifikie kwenye migongano,"alisistiza Meya Shiloo.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Spora Liana amesema halmashauri hiyo itatoa taarifa ya kila matumizi ya fedha yanayofanywa kwa wananchi lengo ni kuweka wazi kwa kila mwananchi kufahamu fedha za maendeleo zinazotolewa kwenye maeneo yao.

Post a Comment

0 Comments