'Ni jukumu lako kujilinda na maafa'

Na Doreen Aloyce,Diramakini Blog

KATIKA kuadhimisha Siku ya Maafa Duniani, Serikali imesema kila mwananchi ajue kuwa ana jukumu la kujilinda yeye mwenyewe pale maafa yanapotokea au kujilinda maafa yasitokee na pia imezitaka taasisi za Serikali na wadau wote kuwa na ushirikiano katika kipindi cha maafa.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kaspar Mmuya mara baada ya ukaguzi wa mabanda ya maonesho kuelekea kilele cha siku ya maafa duniani yaliyopo katika viwanja vya Nyerere jijini hapa.

Amesema, wananchi wengi wanapotoea bila kujua dhamana ya maisha yao wanayo wao wenyewe na kusema kwa kutumia maadhimisho hayo wakusanye taarifa ya kutosha kwa wananchi ili mahitaji yajulikane yapo eneo gani na ni wangapi hawana uelewa wa kutosha.

"Mara nyingi natoa mifano tu, sijui kwa sababu ya kukosa uelewa wa kutosha au kutokukubali kubadilika, mfano lori linapopata ajali watu wanakimbilia kuchukua mafuta matokeo yake mwingine anachukua mafuta mwingine betri hatima yake moto unatokea elimu iwafikie kila mmoja wetu isiwe ndo mwisho kesho shughuli ya kutoa elimu iwe endelevu,"amesema Mmuya.

"Niseme kwamba ni eneo gani la kufanyia kazi ninaamini kutakuwa na kampeni ya nyumba kwa nyumba, kampeni ya mkoa kwa mkoa, kamati zetu za wilaya za mkoa na kitaifa zote zifanye kazi kwa umoja wetu ili tuweze kuzuia madhara ambayo yanatokana na maafa,"amesema Mmuya.

Aidha, amesema ushirikishwaji wa jamii katika masula ya upunguzaji wa maafa katika siku ya kutokomeza na kupunguza maafa duniani ametembelea mabanda 10 na kupata maelezo zaidi jinsi gani walivyojiandaa katika wiki hii ambayo leo tarehe 13 ndio kilele chake.

"Lamsingi nililoliona ni mshikamano katika taasisi zetu za Serikali na wadau mbalimbali ambao wametuunga mkono kwa dhana hii ya maafa nimeweza kujifunza kupata tofauti ya majanga na maafa, maafa ni matokeo na janga ndio matokeo wito wangu kwa wananchi ni kwamba janga la maafa si la ofisi ya Waziri Mkuu peke yake kazi yake ni kuratibu na wadau wengine wa kimataifa,"amesema Mmuya.

Kwa upande wake Winifrida Ngowi mratibu wa maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amesema, maadhimisho ya siku ya maafa duniani huadhimishwa kila tarehe 13 Oktoba na kama Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa maadhimisho haya katika mkoa wa Dodoma, lakini pia kitaifa yamefanyika Chato.

"Katika maadhimisho haya tumefanya shughuli mbili kuu ya kwanza utoaji wa elimu kwa vyombo vya habari ambapo katika vyombo hivi vya habari tumewashirikisha wadau wetu mbalimbali wa maafa hapa nchini ambapo kwenye maadhimisho haya tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii ana kwa ana tukimuelimisha kila mwananchi aliyeshiriki katika maadhimisho haya,"amesema Winifrida.

Amesema, katika suala la ushirikiano wa wananchi Serikali na wadau mbalimbali kwenye usimamizi wa maafa wameshirikisha wadau mbalimbali na pia wamekuwa na zoezi la uchangiaji wa damu ambapo wamefanikiwa kuchangia damu salama chupa 21 na wananchi wanaendelea kujitokeza kuchangia.

"Lakini pia kumekuwepo na shughuli ya utoaji chanjo ya Uviko-19 ambapo inatolewa hapa hapa uwanjani na inatolewa baada ya mwananchi kupata elimu ya umuhimu wa chanjo hiyo,"amesema Winfrida.

Hata hivyo, amesema wameweza kuungana na wadau wengine mbalimbali wa maafa ambao wameshiriki na wanatoa elimu katika maonesho hayo.

"Wadau wenyewe ni Wizara ya Kilimo, Baraza la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, lakini pia kuna taasisi za elimu kama chuo kikuu cha Dodoma, chuo cha Aridhi na chuo cha takwimu cha Afrika na chama cha msalaba mwekundu Tanzania ambao ndio wadau wakuu wa suala la maafa na tunashirikiana nao sana katika shughuli za kupunguza maafa, kujiandaa kukabiliana pindi maafa yanapotokea, pia tuna Shirika la Chakula Duniani (WFP) na wadau wetu wa Plan International,"amesema Winfrida.

Post a Comment

0 Comments