Rais Samia amtoa machozi Mwalimu Makuru, ni kwa kufanya makubwa Mwalimu Julius K.Nyerere University Of Agriculture and Technology (MJNUAT)

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, Mwalimu Makuru Lameck Joseph amejikuta akitokwa na machozi ya furaha baada ya kubaini kuwa,Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetafuta fedha kutoka kwa wafadhili na kutenga zaidi ya shilingi bilioni tisini katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Julius K.Nyerere.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Picha na Maktaba).

Chuo Kikuu cha MJNUAT (Mwalimu Julius K.Nyerere University of Agriculture and Technology) ambacho makao yake makuu yapo mjni Butiama mkoani Mara, kwa mujibu wa kada huyo, Rais Samia ameamua kukiboresha ili kiwe cha kisasa kwa ajili ya kutoa elimu bora, jitihada ambazo zinaenda sambamba na kumuenzi muasisi wa Taifa letu, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

"Haya machozi yamenitoka kwa sababu ya furaha, hiki chuo ni kielelezo tosha cha kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, chuo kilionekana kusuasua kwa kukosekana kwa usajili wa kudumu na kutokamilika kwa miundombinu. Sisi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), nikiwemo mimi (Mwalimu Makuru) ambaye ninapenda kuona ustawi wa elimu kuanzia ngazi za chini hadi juu, nilikuwa ninaumia sana, ila baada ya kutafiti, nimepata majibu kuwa, Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amepambana na anataka chuo hiki kikubwa ambacho kipo kule Butiama kinakamilika, Mwenyenzi Mungu ambariki sana kwa moyo huo wa upendo kwa jamii na Taifa letu, tuna furaha sana kwa hatua hiyo,"amesema Mwalimu Makuru.
Hayo yamesemwa na Mwalimu Makuru mjini Musoma wakati akizungumzia namna ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita inavyozidi kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo ya elimu nchini.

Mwalimu Makuru amesema, kwa hatua hiyo Serikali imeona kuna umuhimu Mkoa wa Mara ukawa na chuo kikuu kikubwa ambacho kitamuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo.

Amesema, hatua hiyo inadhirisha wazi kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza kasi kupambana na adui Ujinga kupitia uwekezaji katika sekta ya elimu nchini.

Ujinga ni miongoni mwa maadui watatu waliotajwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tangu tunapata Uhuru mwaka 1961 huku maadui wengine wakiwa ni Umaskini na Maradhi.
Ikiwa ni kumbukizi ya miaka 22 ya Baba wa Taifa tangu Mwalimu Julius Nyerere azikwe kijijini kwake Butiama mkoani Mara Oktoba, 1999 baada ya kufariki Oktoba 14, 1999, Serikali imekuwa mstari wa mbele kuinua Sekta ya Elimu ili kuwapatia Watanzania elimu bora ambayo itawavusha hatua moja kwenda nyingine.

"Tutaendelea kumuombea sana Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan,kwani yeye anatekeleza mambo makubwa kwa vitendo kimyakimya, huu ni uzalendo wa hali ya juu sana. Mheshimiwa Rais ameamua kukipa heshima ya kipekee chuo hicho huko Butiama ambapo kitakuwa na vyuo vishiriki au matawi matatu, hii ni hatua njema sana,"amesema Mwalimu Makuru.

Mwalimu Makuru amesema, juhudi za Rais zinawezesha tawi moja litajengwa wilayani Serengeti ambapo litajihusisha na kozi za mifugo na wanyama pori (wildlife) na tawi lingine litajengwa wilayani Rorya ambalo litajihusisha na uvuvi,pia wilayani Bunda watajenga tawi ambalo litajihusisha na kutoa kozi za ualimu.

"Hivyo ujenzi wa Chuo cha Kilimo,Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere wilayani Butiama mkoani Mara ni mafanikio makubwa, kiukweli wananchi watafaidika sana sana na mzunguko wa pesa utaongezeka kwa kiasi kikubwa kwa watu na wananchi kwa ujumla ndani ya mkoa wetu wa Mara.Pia kutafungua katika jamii fursa za kimtazamo wa kifikra ndani ya jamii zetu kwa kuthamini elimu,"amesema.

Wakati huo huo,Mwalimu Makuru amesema Serikali kupitia miradi yake mikubwa ya maji ya Mugango kwenda Butiama ambayo imegharimu zaidi ya bilioni sabini na moja itakuwa imeondoa kero kubwa ya maji kwa wananchi mjini Butiama.

Amesema, hatua hiyo itafanya Wilaya ya Butiama alipozaliwa Mwasisi wa Taifa wananchi wake waweze kunufaika na huduma za maji safi na salama,hivvo kuweza kuchochea maendeleo kwa wananchi kama jitihada za kuuenzi mchango wa Baba wa Taifa katika taifa letu la Tanzania.

"Pia Rais Samia Suluhu Hasan Suluhu amezidi kuonesha kwa vitendo kumuenzi Baba wa Taifa ambapo ametenga Bilioni Thelathini na Tano katika ujenzi na ukarabati wa uwanja wa ndege wa Musoma,kusudi kuufanya Mkoa wa Mara kwa ujumla uweze kufunguka kiuchumi hususani katika suala zima la utalii, kwani litawaongezea wananchi kipato cha mtu mmoja mmoja na pato la mkoa kwa jumla,hivyo ujenzi huo utasaidia hata wageni wengi watakaokuja kutalii kuutumia uwanja huo moja kwa moja kuliko kutua kwingine, pia wanachuo kutoka nje ya nchi na mikoa mingine watautumia kwa kutua moja kwa moja katika makao Makuu ya Mkoa mjini Musoma.

"Ujengaji wa Chuo cha Kilimo, Sayansi na Tekenolojia cha Julias Nyerere kitaongezea mkoa wataalamu katika kilimo, sayansi na teknolojia kwanza kuongeza zana nyingi za kilimo na pia wataalamu wengi wataongezeka na uzalishaji nao utaongezeka katika ufugaji na kilimo kwa kupata mbegu bora za mazao ya mifugo na mbegu bora za mazao ya kilimo kwa kuvumbua na kutengeneza zana za kilimo hususani zana za kupandia, zana za kuvunia na zana za kilimo za umwagiliaji,hivyo itaongeza tija sana katika kilimo na kuleta tija katika uzalishaji ndani ya mkoa wetu na nchi kwa ujumla,"amebainisha Mwalimu Makuru.

Mbali na hayo,Mwalimu Makuru amesema Mkoa wa Mara ili uweze kuendelea kiuchumi, viongozi hawana budi kuhakisha suala la utalii wanalipatia kipaumbele,kwani inasikitisha sana kuona Mkoa wa Mara hakuna shughuli za utalii wakati wana mbuga kubwa ya Serengeti ambayo ni miongoni mwa mbuga bora duniani na ni urithi wa Dunia.

"Pia mkoa umezungukwa na fukwe nzuri sana za Ziwa Victoria kuanzia Wilaya ya Musoma Mjini hadi Musoma Vijijini,hivyo viongozi wa mkoa wanatakiwa kuwa wabunifu kwa kuleta wawekezaji katika utalii kusudi mzunguko wa pesa uweze kuongezeka kwa wananchi,"amesema.

Post a Comment

0 Comments