Simba SC washindwa kupumua kwa Coastal Union, Yanga SC wazidi kupaa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mbio za Wekundu wa Msimbazi, Simba SC katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara (Ligi Kuu ya NBC) zimeendelea kuonyesha hali ya ukakasi baada ya mabingwa hao kuonekana kushindwa kumudu kasi.

Ni baada ya leo Oktoba 31, 2021 wakiwa katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam kushindwa kupenya kwa wagosi wa kaya Coastal Union.
Simba imelazimishwa sare kwenye mchezo huo ambao ulikuwa mchezo wa aina yake hasa timu zote mbili katika kipindi cha kwanza kucheza kwa kushambuliana japo kwa upande wa Simba walionesha hamu ya kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Aidha, kipindi cha pili Simba SC ilirudi ikiwa imejipanga kwani walitawala mchezo huo licha ya kutokutumia nafasi nyingi za wazi walizozipata.

Hayo yanajiri baada ya jana watani zao katika dimba hilo Yanga SC kupitia Fiston Kalala Mayele na Jesus Ducapel Moloko kuwapa Wanajangwani ushindi wa 2-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Vijana hao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dakika ya 36 alianza Mayele kuzichakaza nyavu za Azam FC baada ya kumalizia kazi nzuri ya beki mzawa, Kibwana Shomari.

Kwa upande wake Moloko alitumia kipindi cha pili ndani ya dakika ya 73 kufanya mashambulizi akimalizia pasi ya mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Sogne.

Yanga SC kwa ushindi huu inafikisha alama 12 baada ya kucheza mechi nne na kuendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa alama mbili zaidi ya Dodoma Jiji FC ambayo pia imecheza mechi moja zaidi.

Post a Comment

0 Comments