Tisa wavamia wavuvi Ziwa Tanganyika na kuwapora

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, watu tisa wanaodhaniwa ni majambazi kutoka katika moja wapo ya vikundi vya waasi nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamewavamia wavuvi wa Kijiji cha Mpasa wilayani Nkasi mkoani Rukwa na kuwapora vifaa wanavyotumia katika shughuli za uvuvi.
Diwani wa Kata ya Mpasa, Privatus Yoram amesema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 29, 2021 majira ya saa 7 usiku ambapo wavuvi hao walikuwa ziwani wakiendelea na shughuli zao.

Yoram amesema kuwa, wavuvi hao waliliona boti likiwafuata kutokea upande wa nchi jirani ya DRC, ambapo lilifika eneo lao huku kukiwa na watu tisa, waliokuwa wamevalia sare za jeshi na kuanza kuwaamuru wafungue injini ya boti walilokuwa wanatumia kwenye uvuvi ili waondoke nayo.

"Majambazi hao walianza kumpiga nahodha wa boti hiyo wakimtaka atoe spana ili wafungue injini waondoke nayo, lakini aliwaeleza kuwa hakuwa na spana, kitendo kilichowakasirisha na kuanza kuwapiga kwa hasira wavuvi wote waliokuwa kwenye boti hiyo,"amesema Diwani huyo.

Ameongeza kuwa,baada ya kuwapiga wavuvi hao kwa muda mrefu wakaamua kuchukua betri la gari wanalotumia kwenye sola panel, taa za sola, simu za wavuvi hao, vifaa ambavyo huwa wanatumia pindi wanapofanya shughuli za uvuvi na kisha kuondoka navyo.

Diwani huyo amesema kuwa, matukio ya ujambazi kwa sasa yameanza kujitokeza katika kipindi cha mwaka huu na hilo ni tukio la pili katika kata yake, matukio hayo yalikuwa yamekoma kutokea kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini sasa yameanza kujitokeza tena.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nkasi ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Peter Lijualikali alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa bali majambazi hayo yaliiba vifaa vidogo vidogo ambavyo wavuvi wanafanyia kazi.

Mkuu huyo amesema kuwa, kutokana na matukio ya aina hiyo kutokea kwenye kata hiyo amewaagiza wanachi wa kata hiyo kuanza ujenzi wa kituo cha polisi na atawapelekea mchoro wa ramani ya kituo cha polisi na kisha serikali itawapelekea polisi kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa raia katika maeneo hayo.

Kwa nyakati tofauti wakazi wa kata hiyo wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, wapo tayari kwa ajili ya kujitolea kwa hali na mali ili kufanikisha ujenzi wa kituo cha kisasa cha polisi ambacho watashirikiana nacho kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news