Vyanzo vya maji vitunzwe-RC Brigedia Jenerali Ibuge

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekagua vyanzo vya maji kwenye miradi ya maji Ndongosi na Liula wilayani Songea na kuagiza vyanzo hivyo kulindwa ili viwe endelevu.

Aidha, Brigedia Jenerali Ibuge amesikitishwa na uharibifu wa vyanzo hivyo unaoendelea kufanywa na wananchi kwa kulima mazao na shughuli nyingine za kibinadamu hali inayosababisha vyanzo hivyo kuwa katika hatari ya kutoweka.Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akikagua chanzo cha maji Igawisenga wilayani Songea katika ziara yake ya kukagua vyanzi vya maji na miradi ya maji inayotekelezwa na RUWASA.

“Naagiza kila kijiji kuitisha mkutano mkuu wa kijiji,kati ya ajenda zake kuu,iwe ni namna gani ya kukabiliana na tabia hii ya kuharibu vyanzo vya maji,nimeona miti inavyoangushwa kama haina mwenyewe,"amesema RC Ibuge.

Hata hivyo, amesema serikali inapenda watu wajipatie kipato kutokana na kilimo,ametahadharisha kuwa shughuli za kinadamu ndizo zinazoathiri vyanzo vya maji.

Ametoa rai kwa watalaam wote wa maji wakiwemo RUWASA na Bonde la Maji la Ziwa Nyasa,waende vijijini ili kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi na kuweka ramani kwenye eneo zima ambalo lenye vyanzo vya maji ambapo ameagiza utekelezaji wa maagizo hayo ufanyike kabla ya Desemba Mosi mwaka huu.

“Tusiseme tuna changamoto ya tabianchi ni sisi wenyewe ndiyo tunaoharibu kwa kukamata miti,kulima hadi kwenye kingo za mito ,tunachoma moto misitu na kuvunja sheria mbalimbali za mazingira,"amesema RC Ibuge.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji ya Kijiji cha Ndongosi na Liula kwa Mkuu wa Mkoa,Meneja RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles alisema mradi wa maji Ndongosi ulisanifiwa kwa zaidi ya shilingi milioni 332.

Hata hivyo, amesema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi milioni 23 ni fedha za maandalizi ya mradi,zaidi ya shilingi milioni 51 ni za usimamizi na zaidi ya shilingi milioni 256 ni fedha za ujenzi wa mradi wa maji.

Ameutaja mradi wa maji Ndongosi ulisanifiwa kuhudumia wakazi wapatao 3,175 wenye mahitaji ya maji lita 119,062.5 kwa siku na kwamba chanzo cha maji kutoka mto Mlaimonga kina uwezo wa kuzalisha maji lita 902,016 kwa siku na kwamba mradi umefikia asilimia 98.

Kuhusu mradi wa maji wa kijiji cha Liula,Mhandisi huyo wa maji amesema mradi huo awali, ulisanifiwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni moja ambapo RUWASA kwa kutumia watalaam wake wa ndani wamefanikiwa kumaliza shughuli zote kwa shilingi milioni 56 ambapo mradi umekamilika na unahudumia watu wapatao 4,320.

Hata hivyo amezitaja changamoto kuu zinazoikabili miradi hiyo ni uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi kwa kuchoma moto hovyo,kulima kwenye vyanzo na kukata miti.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news