Walimu 51,000 walioshushwa madaraja watolewa hofu, Katibu Mkuu CWT afunguka

Na Robert Kalokola,Geita

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif amewataka walimu zaidi ya 51,000 walioshushwa madaraja yao ya mishahara mwaka 2017 kwenye zoezi la kuhakiki vyeti mwaka huo kuwa wavumilivu kwa sababu chama hicho kimeshawasilisha maombi maalum serikalini na yameshafika kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Deus Seif ameeleza kuwa, mwaka 2015/2016 Serikali ilipandisha madaraja watumishi wa umma zaidi ya 59,000 ikiwemo walimu 51,000 ambao walipewa barua za kupanda madaraja, lakini mwaka 2017 wakati wa kuhakiki vyeti walimu hao walinyang’anywa barua hizo na kuandikiwa barua mpya za mwaka 2017.

Deus Seif katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani wilayani Bukombe ambayo yaliratibiwa na Mbunge wa Jimbo hilo na Waziri wa Madini, Dkt.Doto Biteko kwa ajili ya kukutana na walimu wote wa wilaya hiyo.

Amesema kuwa, CWT imefanya vikao viwili na Ofisi ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na imekubali kupokea maombi hayo na kuyapeleka kwa Rais Samia Hassan, hivyo chama hicho kina imani kubwa kuwa Rais Samia atatatua kero hiyo ya walimu ya madaraja yao.

Ameeleza kuwa chama hicho kinaamini Rais Samia Suluhu Hassan ataifanyia kazi changamoto hiyo kwa sababu imeshapelekwa mezani kwake kwa ajili ya kutatuliwa ili walimu waweze kupata haki yao ya madaraja hayo na kuwaomba walimu wawe wavumilivu.

Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu uadhimishwa kila mwaka Oktoba 5, Duniani kote kufuatia azimio la Shirika la Kazi Duniani na Shirika la Elimu Duniani mwaka 1966 ikiwa la kuleta usawa katika kupata ajira,kuandaliwa pamoja na haki zao.

Ameeleza kuwa, baada ya walimu hao kupewa barua hizo ,serikali imetoa mwongozo wa kupandisha madaraja watumishi mwaka huu,hivyo walimu hao 51,000 wamejikuta wanakosa sifa za kupandishwa madaraja kwa sababu walijikuta hawana sifa ya miaka mine tangu walipopandishwa daraja la mwisho.

Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif anaeleza kuwa licha ya kushushwa madaraja yao kuna walimu ambao mwaka huu wanastaafu hivyo hatua zisipochukuliwa haraka walimu hao wanastaafu wakiwa na madaraja ya nyuma badala ya kuwa na madaraja mapya.

Siku ya Walimu Duniani Kiwilaya imeadhimishwa wilayani Bukombe kwa kuandaliwa na Waziri wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo,Dkt. Doto Biteko kwa ajili ya kutambua mchango wa mwalimu katika maisha yake.

Waziri Biteko ametumia siku hiyo ya mwalimu Duniani kutoa zawadi maalum kwa walimu wake watano ambao alisema walitoa mchango wa peke katika maisha yake ambao wote ni walimu wastaafu na kwa sasa wanaishi maeneo mbalimbali hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news