Wananchi 22,286 wapatiwa chanjo ya UVIKO-19 mkoani Pwani

Na Rotary Haule,Kibaha

WANANCHI 22,286 waliopo mkoani Pwani wamejitokeza kuchanjwa chanjo ya Covid -19 ikiwa sawa na asilimia 75 ya chanjo 30,000 zilizopokelewa mkoani humu.
Mratibu wa chanjo Mkoa wa Pwani Abbas Hincha( kushoto) akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari ofisini kwake Tumbi Mjini Kibaha waliotaka kujua mwenendo wa chanjo ya COVID-19. (Picha na Rotary Haule).

Mratibu wa chanjo Mkoa wa Pwani, Abbas Hincha,alieleza hayo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake waliotaka kujua hatua iliyofikiwa dhidi ya utoaji wa chanjo hizo.

Hincha,alisema kuwa ongezeko la watu kujitokeza kuchanjwa chanjo dhidi ya COVID -19 limekuwa kubwa kiasi ambacho inapelekea kuwa na upungufu mkubwa wa chanjo hizo.

Alisema kuwa , ongezeko hilo linatokana na utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa Harakishi na Shirikishi juu ya utoaji wa chanjo ya COVID -19 ambayo inahusisha mambo mbalimbali muhimu.

Alisema ,moja ya mambo hayo ni pamoja na utoaji elimu kwa jamii katika ngazi mbalimbali hadi kufikia ngazi za chini pamoja na utoaji chanjo hiyo kwa njia ya Mkoba inayohusisha nyumba kwa nyumba,Vijiwe vya boda boda na Kahawa.

Aidha,Hincha aliongeza kuwa jambo lingine ni kuongeza idadi ya vituo vya kutolea chanjo hiyo kutoka 27 vya awali mpaka kufikia 287 hali ambayo imewarahisishia wananchi kufika vituoni kwa urahisi zaidi.

Alisema ,hadi kufikia Oktoba 5 chanjo zilizobaki vituoni ni chini ya 5000 ambazo matarajio yake ni kwamba zitamalizika ndani ya siku mbili huku vituo vingine vikiwa havina chanjo.

" Uhitaji umeongezeka sana kutokana na hamasa inayotolewa kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo ya COVID-19 na sasa tunahitaji chanjo nyingi zaidi ili kuweza kuwafikia wananchi wetu," alisema Hincha

Hincha alisema jambo kubwa wanaloendelea kulifanya ni kutoa elimu kwa makundi ambayo hayajafikiwa ili kusudi waweze kuelimika na hivyo kukubali kuchanjwa.

Hatahivyo,Hincha alisema kwasasa wanasubiria kuletewa chanjo nyingine na mara zitakapofika kila mwananchi mwenye utayari atachanjwa ambapo amewaomba wananchi kuendelea kujitokeza kwakuwa umuhimu wa chanjo hiyo ni mkubwa .

Post a Comment

0 Comments