MHASIBU MKUU TUGHE ANG'ARA KATIKA UCHAGUZI ,WAJUMBE WAMJAZIA KURA

Na Rotary Haule,Dodoma

ALIYEKUWA Mhasibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania(TUGHE) Rugemalira Rutatina ameibuka kidedea kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho katika uchaguzi uliofanyika juzi Mjini Dodoma.
Aliyekuwa mhasibu wa TUGHE Rugemalira Rutatina (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na mwenyekiti mstaafu wa TUGHE Archie Mntambo ( kushoto)kabla ya kuchaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa,katika uchaguzi uliofanyika juzi Mjini Dodoma. (Picha na Rotary Haule).

Rutatina, ameibuka kidedea akiwa ameongoza kwa kupata kura 106 kati kura za wajumbe halali 147 na kuwaacha wenzake wanne wakiwa nyuma kwa kupata kura pungufu.

Awali kabla ya uchaguzi wa nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu kulitanguliwa na chaguzi mbalimbali ikiwemo nafasi ya kamati ya Wanawake Taifa,nafasi ya mwenyekiti Taifa,Makamu mwenyekiti Taifa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa.

Katika uchaguzi huo nafasi ya Unaibu Katibu Mkuu iligombewa na watu watano lakini waliokuwa wanatakiwa katika nafasi ni watu wawili ambapo Rutatina alikuwa kinara kwa kupata kura nyingi zaidi ya wagombea wenzake.

Wengine waliogombea nafasi hiyo ni Amani Msuya aliyekuwa anatetea nafasi yake (73),Jane Mbura aliyekuwa akitetea nafasi yake(49),Dr.Peter Kibacha (9), na Ethel Kaluhuba (49)lakini waliofanikiwa kupata kura nyingi ndio waliofanikiwa kuingia katika nafasi hiyo.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi Andrew Mwalwisi , alimtangaza Rutatina kuwa mshindi kwa kupata kura 106 akifuatiwa na Amani Msuya aliyepata kura 73 na kufanikiwa kutetea nafasi yake.

Kwa mujibu wa Mwalwisi , alisema washindi hao wawili wanakwenda kukitumikia chama hicho katika pande Kuu mbili ambapo mmoja atakuwa Naibu Katibu Mkuu upande wa Serikali na mwingine atakwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu upande wa afya.

"Kwa mamlaka niliyopewa ya kusimamia uchaguzi huu namtangaza Rugemalira Rutatina kuwa mshindi wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu pamoja na Amani Msuya ambapo wote watafanyakazi ya Naibu Katibu Mkuu kwa nafasi tofauti,"alisema Mwalwisi

Aidha,katika nafasi nyingine Afisa Tawala wa TUGHE Steven Wardi , amechaguliwa kuwa mjumbe wa baraza kuu Tucta kwa kupata kura 91 na hivyo kufanya kuwa miongoni mwa wajumbe 16 watakaoingia Tucta wakitokea TUGHE.

Kwa upande wa nafasi ya wadhamini wa chama Mwalwisi, alisema waliochaguliwa ni Albert Mwombeki,Athumani Mokiwa,Zainabu Mwagala na Sekela Mwaijibe .

Wakizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa washindi Rutatina aliwashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumpa kura nyingi huku akiahidi kufanyakazi ya kulinda maslahi ya chama na wanachama wake na hasa katika kutetea kero zao.

Msuya, alisema amekaa miaka mitano katika nafasi hiyo lakini wajumbe wamemuamini tena kwa kumpa miaka mitano mingine na kusema hatowaangusha na kwamba wategemee mazuri zaidi .

Post a Comment

0 Comments