Waziri Jafo afunguka kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

SERIKALI imetoa tamko kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya mkutano wa 26 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Suleman Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamko hilo huku akisema Tanzania hutumia asilimia 2 mpaka 3 ya pato la taifa katika kukabiliana na madhara ya tabianchi.

Waziri Jafo amesema, fedha hizo ni nyingi huku ukizingatia hali ya uchumi wa Tanzania na vipaumbele vya serikali katika kuleta maendeleo kwa watu wake.

Amesema, mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa limetoa taarifa inayothibitisha kuwepo kwa ongezeko la joto katika uso wa Dunia ambapo kuongezeka kwa kiwango cha joto kumesababisha athari za mabadiliko ya Tabianchi katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

"Athari hizo ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kulikosababisha kisiwa cha maziwa Wilaya ya Pangani na kisiwa cha fungu la Nyani Wilaya ya Rufiji kumezwa na maji ya bahari.

"Katika msimu wa mwaka 2019 mpaka 2020 mvua zilisababisha kuongezeka kwa kina cha maji kwenye ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika huku miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mafuriko ya mara kwa mara na ukame wa muda mrefu kwenye baadhi ya maeneo nchini,"amesema Waziri Jafo.

Amesema, pamoja na ukweli kwamba Tanzania sio miongoni mwa nchi zinazozalisha gesi joto kwa wingi duniani serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo kujenga uwezo wa kitaasisi kutoa elimu kwa jamii na kuhimiza shughuli za kilimo,ufugaji na uvuvi zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Katika mkutano huo Tanzania itashirikiana kikamilifu katika majadiliano ya masuala yenye maslahi mapana kwa nchi yetu na kuweka misimamo wake kwa yafatayo Rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mkataba na makubaliano ya Paris, kujenga uwezo, kilimo na mabadiliko ya tabianchi ,uendelezaji na usambazaji wa teknolojia,mchango wa taifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,upunguzaji gesi joto kwa kutumia biashara na jinsia na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba huo utafanyika jijini Glasgrow nchini Scotland kuanzia Oktoba 31 mpaka Novemba 12, mwaka 2021 na utahudhuriwa na wajumbe 3000 kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo wakuu wa nchi na serikali,mawaziri na wataalam waliobobea katika masuala ya tabia ya nchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news