Waziri Mchengerwa arejesha tabasamu kwa walengwa wa TASAF Kata ya Nyamatongo

Na James K. Mwanamyoto-Sengerema

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaelekeza Waratibu wa TASAF wilayani Sengerema kuwaandikisha walengwa wenye sifa ya kunufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya maskini katika kata ya Nyamatongo ambao walisahaulika wakati wa zoezi la uhakiki na uandikishaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akilakiwa na wananchi na wanufaika wa TASAF wa Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo akiwa Wilayani Sengerema Kata ya Nyamatongo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.

Katika kuhakikisha anatimiza azma ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuzifikia kaya zote maskini nchini, ameutaka uongozi wa Wilaya, Mkoa na TASAF Makao Makao kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kujiridhisha na utekelezaji wa agizo lake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF wa Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.

“Waandikisheni wote wanaodai kusahaulika na mhakikishe mnajiridhisha kama wana sifa za kuwa walengwa na mniwasilishie taarifa ya utekelezaji wa agizo langu ndani ya wiki mbili,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ameongeza kuwa, ndani ya wiki hizo mbili Waratibu wahakikishe wanafanya mapitio ili kujiridhisha kama waliojiandikisha wamekidhi vigezo na sifa za kuwa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali.
Sehemu ya wananchi na wanufaika wa TASAF wa Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na wananchi na wanufaika wa TASAF wa Kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani humo.
Mmoja wa Maafisa wa Kata ya Nyamatongo, Wilaya ya Sengerema akiandika majina ya wananchi ambao wanadai kusahaulika katika zoezi la uandikishwaji wa wanufaika wa baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kutoa maelekezo ya uandikishwaji wa wananchi hao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Sengerema.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wa kata ya Nyamatongo kuendelea kuwa na imani na Serikali ya Awamu ya Sita, kwani ofisi yake itaendelea kutekeza jukumu la usimamizi wa TASAF kikamilifu ili kuunga Mkono kwa vitendo kaulimbiu ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya KAZI IENDELEE.

Kwa upande wake, Mbunge wa Sengerema Mhe. Tabasamu Hamisi amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa hatua hiyo na kuongeza kuwa, kaya maskini ambazo hazijaandikishwa zimeibua malalamiko katika jimbo analoliongoza.

Kufuatia hatua iliyochukuliwa na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa TASAF, Mhe. Tabasamu amewahakikishia wananchi wa jimbo lake kuwa walengwa wote waliosahaulika wataandikishwa kama ambavyo Mhe. Mchengerwa ameelekeza.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema, Mhe. Tabasamu Hamisi akielezea hali ya utekelezaji wa TASAF katika Jimbo lake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Sengerema.

Mhe. Tabasamu amesema, jimbo la Sengerema na Buchosa lina wazee zaidi ya elfu tisini lakini wazee wanaonufaika na mpango wa TASAF hawazidi elfu kumi na tatu hivyo agizo la Mhe. Mchengerwa ni muafaka wa changamoto hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amefanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF wilayani Sengerema, mara baada ya Mbunge wa Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu kuwasilisha malalamiko ya wananchi wa jimbo lake kutoandikishwa kwenye mradi wa TASAF.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news