Chifu Mugenyi Senge Mugenyi Ndovu asimikwa kuwa Chifu Mkuu Singida

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

UMOJA wa Machifu Mkoa wa Singida umewaomba wana umoja huo kufanya zoezi la kuwasimika machifu wengine katika maeneo yao kabla ya kwenda kushiriki mkutano mkuu wa machifu Tanzania utakaofanyika mkoani Kilimanjaro.
Ikiwa ni katika maandalizi ya kujiandaa kukutana na Mkuu wa Machifu Tanzania, Chifu Hangaya ambaye ni Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Mkoa wa Singida, Chifu Mjengi Gwau ameyasema hayo wakati akizungumza katika hafla ya kumsimika Mkuu wa Machifu Mkoa wa Singida, Chifu Mugenyi Senge Mugenyi Ndovu.

Pia amewataka kushirikiana ili kutimiza malengo huku akitoa rai ya kuundwa kwa mabaraza ya wazee watakaosimamia mila na desturi za Kitemi mkoani hapa."Na wengine wote tusaidiane ili wafanye haya, tunangojwa kwenda kufanya mkutano wa Umoja wa Machifu Tanzania huko Marangu, Moshi ili tuchague viongozi wa umoja wa machifu, tukishamaliza Chifu Hangaya anatuita machifu wote Dodoma, halafu tutaunda mabaraza ya wazee yatakayosimamia mila na desturi zetu,"amesema Chifu Mjengi.

Aidha, baada ya kusimikwa kuwa Mkuu wa Machifu Mkoa wa Singida, Chifu Mugenyi Senge Mugenye Ndovu ameshukuru kupata nafasi hiyo na kueleza kuwa atakuwa ni kiunganishi kati ya Serikali na jamii katika kufanikisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
"Mimi nimefurahi sana kwa kutawazwa kuwa chifu, kuna miradi mingi sana ambayo Serikali imekuwa ikitoa, lakini wananchi stahiki wanaotakiwa kupata walikuwa hawapati kwa sababu hakukuwa na mtu wa kuwatetea, imekuwa ni nafasi nzuri ya mimi kuwatetea kwa sababu nawajua raia. Mimi nitakuwa kiunganishi kati ya Serikali na jamiii,"amesema Chifu Mghenyi Senge Ndovu.

Pia kuhusu migogoro ya ardhi, chifu huyo ameeleza namna ambavyo umilikishaji usiohalali unavyopelekea migogoro na kuiomba Serikali kushirikiana katika kuitatua huku akitoa shukurani kwa Mkuu wa Machifu Tanzania, Chifu Hangaya ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

"Kuna baadhi ya watu ambao wametoka katika mikoa mingine wametumia njia za ujanja ujanja kumiliki maeneo makubwa ya ardhi.
"Sisi tutasimama kuhakikisha wananchi wanapata haki zao, kwanza nimpongeze Chifu Hangaya , wakati anasimikwa kuwa Mkuu wa Machifu Tanzania nilikuwa miongoni mwa machifu niliokuwepo kwenye tukio hilo na hii inaonesha utamaduni na mila zetu zinaheshimika,"ameongeza Chifu Ndovu.

Kwa upande wake, Katibu wa Chifu Ndovu amabaye pia ni mtoto wake, Salum Mghenyi Ndovu amesema mkuu huyo wa machifu atasimamia maeneo ya asili kama vile misitu na vyanzo vya maji.

"Kuna mambo mengi sana ambayo chifu atayasimamia zamani tulikuwa na maeneo yetu ya asili kama vile msitu, vyanzo vya maji ambayo kwa sasa havizingatiwi sana kuna maagizo alitoa Katibu wa Wizara ya Sanaa Utamaduni, Dkt.Hassan Abbasi kuwa machifu waorodheshe maeneo yao yalikuwa ya kiutawala wa kichifu, hivyo kuna maeneo hapa Singida yanahitaji usimamizi wa chifu na ndio kazi ambayo ataifanya,"amesema Katibu huyo.

Hata hivyo, Mkoa wa Singida una jumla ya machifu sita ambao huongoza shughuli mbalimbali za Kitemi kama mila na desturi ya jamii yao kwa lengo la kuendelea kulinda na kuzitunza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news