DC Mwaipaya awataka wazazi kusimamia maadili ya watoto

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WAZAZI wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro wametakiwa kusimamia maadili ya watoto wao badala ya kuwaachia walimu peke yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdalah Mwaipaya wakati wa mahafali ya Kidato cha Nne katika Shule ya Vuchama Ugweno Islamic.

Mwaipaya amesema kuwa, ili wanafunzi waweze kufanya vyema kwenye masomo yao lazima kuwe ushirikiano baina ya wazazi na walimu.

Amesema kuwa, wazazi nao wanasehemu ya ufaulu wa wanafunzi hivyo nao wanapaswa kushiriki kwa kuwafuatilia masomo yao na si kuwaachia walimu peke yake.

Aidha, amewataka wanafunzi hao wanaomaliza elimu ya sekondari wazingatie maadili mema wanayofundishwa shuleni ili kuwa na Taifa na viongozi bora.

"Maadili mliyoyapata muende nayo msije mkabadilika na kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa na kusababisha kufanya vibaya kwenye masomo na kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho,"amesema Mwaipaya.

Katika hatua nyingine amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanalipa ada kwa wakati ili shule hizo ziweze kujiendesha kwani zinategemea ada kama sehemu ya kujiendesha na hazina ruzuku.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo, Jumanne Mkoga amesema kuwa, changamoto kubwa shuleni hapo ni kukosa uzio hali ambayo inasababisha kuwe na muingiliano na watu wasio wanafunzi.

Mkoga amesema kuwa, muingiliano huo husababisha wizi na kuingiza kwa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na dawa za kulevya kama bangi na kufanya vitendo vibaya.

Awali meneja wa shule hiyo, Yasin Mfinanga amesema wanaomba ushirikiano na serikali ili kuwapatia wanafunzi kwani wao wana madarasa ya kutosha tofauti na shule za serikali ambazo zina upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mfinanga amesema kuwa, ili kuboresha sekta ya elimu ni vema kukawa na ushirikiano baina serikali na sekta binafsi kwa kuwapunguzia wanafunzi wanaokosa nafasi.

Post a Comment

0 Comments