Kilindi yaweka mradi wa kufyatua matofali kuharakisha miradi

NA YUSUPH MUSSA

Katika kukabiliana na miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya madarasa na vituo vya afya, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, wameweza kununua mashine mbili zenye thamani ya sh. milioni 16 kwa ajili ya kufyatua matofali.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wakiwa kwenye kikao.

Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imepata fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 131 kwa ajili ya shule za msingi Shikizi na vyumba vya madarasa 65 kwa ajili ya sekondari, huku wakijenga Kituo cha Afya Tunguli kilichopo Kata ya Tunguli, Tarafa ya Kwekivu. Pia Kituo cha Afya Mswaki kilichopo Tarafa ya Mswaki.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Gracian Makota ameyasema hayo wakati akizungumza na DIRAMAKINI BLOG juu ya ni namna gani mashine hizo zitasaidia kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, kwani Januari mwakani, wanatakiwa kuwapeleka kidato cha kwanza wanafunzi wote watakaofaulu,kwa kuwa hakutakuwa na chaguo la pili.

"Kutokana na halmashauri yetu kuwa na miradi mikubwa ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vituo vya afya, imebidi tununue mashine ili kuweza kuwa na mradi wa kutengeneza matofal. Mradi huo utatuwezesha kufyatua matofali kwa uhakika ili kuendana na ujenzi wa vyumba vya madarasa 131 ya shule za nsingi Shikizi, na madarasa 65 ya shule za sekondari.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Idrissa Mgaza akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Seiya Ndeiya Keiya.

"Lakini pia tuna mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Tunguli na Kituo cha Afya Mswaki. Hivyo mradi huo wa matofali utakuwa wa kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Na ndiyo maana tunatafuta jenereta ambazo zitasaidia zoezi hilo sababu huko tunakokwenda kujenga miradi hiyo maeneo mengi hayana umeme wa uhakika, hivyo itasaidia kazi kufanyika kwa ufanisi," amesema Makota.

Makota amesema miradi yote hiyo ni muhimu, lakini Kituo cha Afya Tunguli kitakuwa ni msaada mkubwa sana kwa wananchi wa ukanda huo kuanzia Kata ya Tunguli yenyewe, Pagwi, Kikunde na Kwekivu, kwani wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanalazimika kwenda Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro kufuata matibabu, huku wengine wakitibiwa kwenye vituo vya afya binafsi ambavyo gharama yao ya matibabu ipo juu.

"Tunashukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwani miradi aliyotuletea ina tija kubwa ikiwemo vyumba vya madarasa kwenye shule za msingi na sekondari, lakini pia vituo vya afya. Lakini Kituo cha Afya Tunguli ni msaada mkubwa zaidi kwa wananchi, kwani wananchi wa kata za Tunguli, Pagwi na Kwekivu walikuwa hawana huduma ya afya ya uhakika, na iliwalazimisha kwenda Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, na bado walikuwa hawapati matibabu ya uhakika.
Diwani wa Kata ya Kikunde, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Amon Ramadhan, akisoma taarifa ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) kwa niaba ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Idrissa Mgaza. Ni kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

Makota amesema, mashine hizo mbili za kufyatua matofali, ambapo pia kuna mashine ya kuchanganya mchanga na saruji, kwa siku zitakuwa na uwezo wa kufyatua matofali 3,000. Na kila mashine moja itaajiri ajira ya muda kwa vijana 20, huku akisema mradi huo ni kwa ajili ya kutoa huduma, na sio biashara. Nia ni kuona miradi waliyokusudia inakamilika kwa wakati.

Wakati huo huo suala la mradi wa kufyatua matofali lilijadiliwa kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Kilindi lililofanyika Oktoba 29,2021 ambapo akisoma taarifa ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM), Diwani wa Kata ya Kikunde Amon Ramadhan, alisema mradi huo wa matofali una manufaa makubwa kwa ajili ya miradi mikubwa ya Serikali.

Akichangia taarifa ya FUM, Diwani wa Kata ya Mvungwe Abdallah Ndalo alisema kwa kuwepo mradi huo, hakuna haja ya kuchelewesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 65 katika shule za sekondari ili wanafunzi watakaochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani waweze kuingia wote darasani.

"Serikali imetupatia fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya elimu na afya, lakini ni matumaini yangu mashine hizi za kufyatua matofali zitafanikisha malengo yetu ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wanaotakiwa kuingia kidato cha kwanza mwakani," alisema Ndalo.

Post a Comment

0 Comments