Dkt.Dugange:Serikali imetumia zaidi ya Bilioni 95/- kununua vifaa tiba

NA FRED KIBANO

SERIKALI imetumia jumla ya shilingi Bilioni 95.37 ambazo zimetumika kununua vifaa tiba na kupelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuboresha afya za wananchi na ustawi wa Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Dkt.Festo Dugange, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Novemba 23,2021 jijini Dar es Salaam wakati akitoa maelezo ya awali kwenye Mkutano wa 22 wa Mapitio ya Sera na mafanikio kwenye Sekta ya Afya ambao unafanyika kila mwaka.

“Serikali imeweza kununua Vifaa Tiba vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 95.37 kupitia fedha ya mkopo nafuu kutoka Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) kwa ajili ya Vituo vya kutolea huduma za Afya katika ngazi ya Halmashauri ” alisisitiza Dkt. Dugange.
Dkt. Dugange amesema, pia halmashauri zinaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya majengo ya Idara ya dharura (EMD) - 80, Wagonjwa mahututi (ICU) - 26, Nyumba za Watumishi 150 katika Vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 44.5 kupitia fedha za Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) ambayo ni mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya.

kuhusu ujenzi wa vituo vya afya amesema hadi kufikia mwezi Novemba, 2021 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilipeleka fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 55.25 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya 221 katika maeneo ya kimkakati kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini.
Akifungua Mkutano wa 22 wa Mapitio ya Sera na mafanikio kwenye Sekta ya Afya, Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima amesema, Serikali katika ngazi ya Msingi imefanikisha kusajili zahanati 5,325, vituo vya afya 629 pamoja na Hospitali za Wilaya 68 ambazo zote zinatoa huduma.

Aidha, vituo vipatavyo 415 vinatoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa mama wajawazito na huduma kwa Watoto wachanga hali iliyoongeza mwamko kwa kina mama kuhudhuria kwenye vituo vya afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe, amesema Serikali inaendelea kuimarishaji mifumo ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na mfum Afya-Care na GoTHOMIS ambayo itasaidia kuimarisha takwimu za afya na mipango ya afya inayopimika kwa kuweka vipaumbele vinavyolingana na takwimu kupitia mifumo hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news