Mradi wa HPSS waimarisha Maktaba Mtandao za Afya

NA ASILA TWAHA

MKURUGENZI wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais - TAMISEMI,Dkt. Ntuli Kapologwe amepokea vifaa vitakavyo imarisha maktaba mtandao za Afya kutoka Mradi wa Uimarishaji wa Huduma za Afya (HPSS) vyenye thamani ya shilingi milioni 17.Akipokea vifaa hivyo Novemba 23,2021 ofisini kwake Jijini Dodoma,Dkt. Ntuli amesema vifaa hivyo vitasaidia watumishi wa Afya kuendelea kupata taarifa ya masuala ya afya kupitia maktaba mtandao nchi nzima.

“Vifaa hivi vitaimarisha maktaba mtandao ili kusaidia wataalam wa sekta ya afya kwa ngazi ya Mkoa na Halmashauri kupata taarifa sehemu moja pale zinapohitajika za utoaji wa huduma za afya,"amesema.

Akifafanua mchango wa Mradi wa Uimarishaji wa Huduma za Afya (HPSS) amesema, umesaidia katika masuala ya usimamizi Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa (iCHF), masuala ya kiufundi (Technical support), Usimamizi wa bidhaa za Afya, “Health Promotion” na matengenezo ya vifaa na vifaa tiba.

“HPSS ulianza kama mradi wa majaribio baada ya kufanya vizuri na kwa mafanikio hayo sasa upo nchi nzima,”amesema Dkt. Ntuli.

Amesema, Serikali inaendelea kuwekeza kwa kujenga na kuboresha miundombinu mizuri ya Afya ya ufanyaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Ameushukuru uongozi wa Mradi wa Uimarishaji wa Huduma za Afya (HPSS) kwa kuendelea kushirikia na Serikali katika kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora kwenye masuala ya afya.

Naye Meneja wa Mradi wa HPSS, Ally Kebby ameishukuru Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa kuendelea kusimamia na kutekeleza afua mbalimbali za afya nchini na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano.

Vifaa vilivyotolewa ni kopyuta mpakato, projekta, printer, photocopy na vingine vitasaidia kuwezesha kukusanya na kuchakata taarifa.

Post a Comment

0 Comments