DR Congo yatinga mtoano Kombe la Dunia Qatar 2022, Taifa Stars yaachwa

NA GODFREY NNKO

DR Congo ambayo iliharibu mipango yote ya Taifa Stars kusonga mbele kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, wamefanikiwa kutinga katika hatua ya mtoano.
Awali, Watanzania walikuwa na matumaini makubwa kwa Taifa Stars kusonga mbele, lakini mipango yote ilivurugwa na Wakongo kwa kuachia kichapo cha mabao 3-0 katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Straika wa DR Congo, Dieumerci Mbokani (35) katika Kundi J ametupia nyavuni mabao manne. (Picha na Getty Images).

Aidha, licha ya Wakongo ambao walionekana kuanza kwa kusuasua Novemba 14, 2021 imemaliza michezo ya hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kucheza hatua ya mtoano ya Kombe la Dunia Qatar 2022 kama vinara baada ya kuichapa bao 2-0 Benin.

Mchezo huo umepigwa katika dimba la Martyrs de la Pentecôte mjini Kinshasa ambapo DR Congo mbali na kucheza vizuri wamevuna alama sita na mabao matano kwenye mechi mbili za mwisho bila kuruhusu goli.

Wafungaji katika mtanange huo kutoka DR Congo ni Straika Dieumerci Mbokani ndani ya dakika 10 katika kipindi cha kwanza, bao ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Aidha, bao hilo liliendelea kuwa mtaji wa DR Congo huku Benin wakitafuta fursa bila matokeo, ambapo dakika ya 75, Ben Malango aliiandikia DR Congo bao la pili, hadi mwisho wa mtanage ubao ulisoma Benin imeambulia patupu.

Kwa matokeo hayo, DRC inamaliza kileleni kwa alama zake 11, ikifuatiwa na Benin 10 na Taifa Stars nane, wakati Madagascar imeshika mkia kwa alama zake nne.

Kongo inakwenda hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Qatar ambako itakutana na mmoja wa washindi wa makundi mengine tisa katika mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atakuwa mmoja kati ya wawakilishi watano wa Afrika Kombe la Dunia 2022.

Wakati huo huo, huko katika dimba la Manispaa la Mahamasina nchini Madagascar, Taifa Stars imeshindwa kuendelea kwenye hatua inayofuata mara baada ya kushindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi za mwisho kwenye kundi lao.

Taifa Stars imelazimishwa sare ya 1-1 na Madagascar kwenye mchezo huo wa mwisho hatua ya makundi kufuzu kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Taifa Stars ilianza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake Simon Msuva dakika ya 25 ya mchezo katika kipindi cha kwanza na kuiwezesha timu yake kuongoza katika kipindi chote cha kwanza.

Aidha, kipindi cha pili timu ya Madagascar ilitawala mchezo ikihitaji kusawazisha goli katika mchezo huo kwani walifanya mabadiliko kadhaa ambayo yaliza matunda japo Tanzania ilikuwa inacheza kwa kujihami zaidi.

Msuva aliwezesha bao hilo ndani ya dakika 25 ya kipindi cha kwanza ambalo lilidumu hadi mapunziko, kipindi cha pili wenyeji wao walianza kusaka fursa ambapo dakika ya 74, Hakim Djamel Abdallah alipashika bao, hivyo ubao kusoma moja moja.

Licha ya jitihada za kila upande matokeo hayo yaliendelea hivyo, ambapo dakika ya 83, Madagascar walicheza pungufu baada ya Pascal Razakanantenaina kupewa kadi nyekundu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news