Mtigandi aweka wazi faida za elimu ya haki ya afya kwa wanawake

NA MARY MARGWE

MAFUNZO ya haki ya afya ya uzazi salama yanayoendelea katika Kata ya Riroda wilayani Babati mkoani Manyara kwa wanawake na wasichana imeelezwa yatawasaidia kuwapa uelewa na kuchukua hatua stahiki iwapo watagundua kufanyia vitendo vya ukatili dhidi yao.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara (MNRPC), Zacharia Mtigandi ameyasema hayo wakati akizungumza mbele ya wanawake, wasichana pamoja na waandishi wa habari wa mkoa huo kupitia mafunzo maalumu..

Amesema, mafunzo hayo yanatarajia kuwafikia zaidi ya wanawake na wasichana 200 kutoka kata tatu ikiwa ni pamoja na Endasaki wilayani Hanang', Kata ya Riroda wilayani Babati.

Mtigandi amesema, mafunzo hayo yatawasaidia kuwapa uelewa iwapo watafanyiwa ukatili wowote ule watajua namna ya hatua zinazoshahili kuchukuliwa juu yao.

"Haya ni mafunzo katika kundi hili la wanawake na wasichana ni kundi ambalo huwa halipewi kipaumbele katika jamii, kwani wanawake wengi wamekua wakitelekezewa kuwahudumia watoto na kuwalea wao binafsi kana kamba mwanaume amekufa, kumbe yupo anaendekeza starehe huku familia akiwa amemuachia mama kulea mwenyewe,"amesema Mtigandi.

Aidha, amesema kupitia sasa mafunzo wanayoendelea kupata yatawasaidia kuwafumbua macho na hatimaye kuweza kuwachukulia hatua pale wanaume watakaposumbua kuilea familia na kutoa mahitaji muhimu.

Aidha, amesema wanawake wanatakiwa kuamka kupinga ukatili wa kinjinsia ili kuwawezesha kuwa na familia salama na hatimaye kuweza kuzalisha kizazi kilichosalama katika jamii inayowazunguka.

Naye mkazi mmoja wa Kata ya Riroda Mariam Habib amesema kila jambo likifanywa baada ya kupata elimu huwa linafanyika kwa ufasaha zaidi kuliko pale lilipofanyika kabla ya kupata elimu, hivyo kwa sasa kila mwanamke amekuwa na utayari mpya juu ya elimu ya haki ya afya ya uzazi salama.

"Elimu tuliyoipata hakika imetuwezesha kwanza kabisa kuwa majasiri na kuweza kuelezea hali ya maisha yetu tunayoishi na wenza wetu huko majumbani mbele ya maafisa afya na maafisa ustawi wa jamii kwani pia mbele ya waandishi wa habari, lakini kubwa ni namna ya kufikisha matatizo yetu katika maeneo yanayotupasa kufikisha matatizo yetu,"amesema Habib.

Aidha, mkazi mwingine wa Kata ya Riroda, Salome Benedict amesema, wanaume wamekua wakiwanyanyasa mara kwa mara bila kosa lolote, "na endapo atakusikia umeenda kumshitaki mahali, utakaporudi utapigwa viboko kana kwamba umefumaniwa, hivyo mafunzo tuliyoyapata yametupa ujasiri wa kupambanua jambo katika maisha,"amesema.

Hata hivyo, mafunzo hayo yalitolewa na Manyara Press Club (MNRPC ) chini ya ufadhili wa Women Fund Trust (WFT) ambapo walitoa Shilingi Milioni 10 kwa klabu hiyo ili kutekeleza mradi huo wa miezi sita katika wilaya ya Hanang' na Babati.

Post a Comment

0 Comments