Maaskofu 120 wa Kanisa Katoliki barani Afrika kukutana nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Zaidi ya Maaskofu 120 wa Kanisa Katoliki kutoka nchi nane barani Afrika wanatarajia kukutana Julai, 2022 hapa nchini.
Kutaniko hilo ni kwa ajili ya kufanya kikao cha kuweka mikakati na maafikiano ya kunusuru Dunia dhidi ya changamoto ya uharibifu wa mazingira.

Aidha, hatua hiyo inakuja baada ya waraka rasmi yaani Laudato si uliotolewa Mei 25, 2015 na kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis.

Waraka ambao umeagiza hatua madhubuti zichukuliwe ili kuinusuru Dunia dhidi ya uharibifu wa mazingira duniani unaosababishwa na shughuli za kibinadamu na kiuchumi.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima ameyasema hayo jiujini Mwanza ambapo amefafanua kuwa, kikao hicho cha siku 10 kitahudhuriwa na maaskofu kutoka nchi nane za Afrika huku ajenda kuu ikiwa ni kuweka mkakati wa kuhakikisha Dunia inalindwa kwa kupambana na uharibifu wa mazingira kupitia upandaji wa miti katika ngazi ya familia. 

"Tunaombwa kama binadamu tukae chini tutafakari namna gani tuyaweke mazingira vizuri yaweze kutufaa sisi na kizazi kijacho, sayari hii ndiyo tuliyonayo, tusipoihifadhi tutakuwa hatarini kwani kuharibu mazingira ni kuharibu uhai wa mwanadamu na viumbe wengine," amesema.

Padri Kitima amesema, kanisa hilo nchini limedhamiria kuifanya Tanzania iwe ya kijani kwa kuanzisha kampeni ya upandaji wa msitu wa familia utakaotoa nafasi kwa mwanafamilia kupanda miti mitatu.

"Tunahimizwa kila familia kuwa na msitu wa familia, kitongoji na kijiji na hatimaye tuwe na misitu ya asili ya kijamii kama wanavyofanya Ethiopia,"amesema Padri huyo.

Aidha, Padri Kitima kupitia Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (Emecea) amesema, kanisa hilo litatoa wataalam wa misitu watakaotembelea kila kaya na familia kutoa elimu ya upandaji miti na matumizi bora ya mazingira.

Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula amelipongeza baraza hilo huku akisema kampeni hiyo itasaidia kuinusuru nchi dhidi ya hatari ya kuwa jangwa.

"Pamoja na kwamba Serikali ina mpango wa kupanda miti 1,500,000 kila wilaya, lakini siyo kwamba yote itapandwa na kukua, lakini kupitia kampeni hii tunaamini ufanisi wa upandaji miti nchini utakuwepo na nchi yetu itakuwa ya kijani,"amesema Dkt.Mabula.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news