Madiwani Namtumbo waibua hoja nzito kuhusu korosho

NA YEREMIAS NGERANGERA

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wameelezea kutoridhishwa na hatua ya Idara ya Kilimo na Ushirika kuruhusu korosho kuuzwa wilayani Tunduru mkoani humo.
Wakiongea kwenye kikao hivi karibuni madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamedai kukosa imani na idara hiyo kutokana na kushindwa kutekeleza maazimio ya kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo na maagizo ya kikao cha wadau wa mazao wilayani humo.

Diwani wa Kata ya Magazini, Grace Kapinga amesema idara ya kilimo na ushirika iliagizwa kuweka mikakati ya kuhakikisha msimu wa korosho 2021/2022 unafanyika katika wilaya ya Namtumbo badala yake wakulima wa zao la korosho katika kata yake na kata zingine wanaendelea kuuza korosho zao Tunduru na kupuuza maamuzi ya vikao vya baraza la madiwani kuwa korosho za wakulima wa Namtumbo ziuzwe Namtumbo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Juma Pandu kwa upande wake alidai upo uzembe wa idara kupuuza maagizo ya vikao vya madiwani pamoja na vikao vya wadau walioamua zao hilo liuzwe wilayani Namtumbo kwa kuwa tunakidhi vigezo .

Pandu amesema kuwa, hapa kuwa na ushirikishwaji wa taarifa juu ya kukwama kwa maagizo ya vikao kuhusu kuuza korosho katika wilaya ya Namtumbo zaidi ya kujionea wakulima wa Namtumbo kuendelea kuuza korosho wilayani Tunduru bila kujua kilichokwamisha zoezi hilo kufanyika Namtumbo.

Afisa kilimo na ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Andrew Tarimo amesema tatizo kubwa lililosababisha ni kukosa wafanyabiashara wenye leseni za maghala ya kununulia zao la korosho wilayani Namtumbo.

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Vitta Kawawa kwa upande wake alidai kitendo cha kuendelea kuuza korosho wilayani Tunduru kinapunguza kasi za uzalishaji wa zao la korosho wilayani Namtumbo na kitendo hicho hakivumiliki.

Kawawa ameongeza kuwa, zao la korosho lingeuzwa Namtumbo kasi za uzalishaji ungeongezeka kwa kuwa wakulima wengi wa zao la korosho hawahudumii korosho zao kutokana na soko kuwa wilaya nyingine ambayo ipo mbali.

Aliitaka idara husika kutekeleza maamuzi ya vikao na kwenye dalili za kutotekelezeka kwa maamuzi ya vikao kunatakiwa kuwepo kwa ushirikishwaji wa viongozi ili kutatua changamoto na kufikia malengo yaliyokusudiwa na vikao.

Madiwani wilayani Namtumbo wamedhamiria kuchukua maamuzi magumu kwa mtumishi yeyote kwenye idara inayokwamisha utekelezaji wa maagizo ya vikao vya madiwani katika halmashauri yao.

Wilaya ya Namtumbo ina zalisha korosho zaidi ya tani 1000 kutoka katika kata zake 21 ambapo korosho hizo husafirishwa umbali wa zaidi ya kilomita 200 kwenda wilayani Tunduru na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wakulima wa korosho wilayani Namtumbo.

Hali iliyoibua malalamiko ya kutaka kuwepo na soko la korosho wilayani Namtumbo bila mafanikio, hali ambayo waheshimiwa madiwani wanaamini ni uzembe wa idara husika katika kusimamia kikamilifu zoezi hilo.

Post a Comment

0 Comments