TPS SACCOS yapewa mbinu za kustawi kiuchumi, kuneemesha wanachama

NA DOREEN ALOYVE

KATIBU Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christopher Kadio ameutaka Uongozi wa Chama cha Ushirikia wa Akiba na Mikopo cha Watumishi wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara (TPS SACCOS) kuwa wabunifu katika uendeshaji na kuhamasisha wengine kujiunga ili waweze kufikia malengo ya pamoja.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Magereza SACCOS uliofanyika makao Makuu Makuu ya jeshi hilo.

Aidha, amesema kuwa viongozi hao wanapaswa kuwa wabunifu namna ya kuendeleza SACCOS yao hasa kwa kuzingatia dhana ya uzalishaji mali ikiwa ni pamoja kutoa elimu ya ushirika jambo ambalo litasaidia kuwa na maendeleo makubwa.

"Niwapongeze sana kwa hatua hiyo na ili chama chenu kiweze kuendeshwa kwa tija lazima kuzingatia Sheria namba Sita ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2015, hivyo simamieni hii SACCOS vizuri,"amesema.
"Pia uongozi wa chama niwasihi kwamba ili chama kiweze kufanya vizuri lazima kipewe kipaumbele huku mkipaswa kuendana na kasi iliyopo hasa kutoa elimu ya ushirika,kushirikisha wanachama juu ya bajeti ya chama,"amesema Kadio.

Nae Ramadhan Mbezi Afsa mikopo wa Chama cha TPS SACCOS amesema kumekuwa na mafanikio mengi huku na wanachama wakijivunia na chama hicho kupata mikopo kwa wakati ambapo mpaka kufikia Oktoba, mwaka huu tayari wanachama 2,258 wamekopeshwa kiasi cha shilingi bilioni 3.3 katika mkopo wa dharura.

Pia amesema, mkopo wa bilioni 8 kwa ajili ya maendeleo kwa wanachama 872 jambo ambalo kinawasaidia kutatua shida zao kwa wakati.
Akielezea changamoto amesema, hapo awali ilikuwa ni urejeshaji wa mkopo wa dharura lakini kupitia elimu ambayo wamekuwa wakiitoa na mfumo wa kupitia kwa mwajiri wao imesaidia kuondoa changamoto hiyo.

"Tuna mikakati mikubwa ni kuhakikisha wanachama wote wanajiunga ambao ni askari wastaafu na wenza wetu na kwa sasa tuko 11,000 huku Jeshi lina askari 12,000 hivyo tunataka kuwafikia wote ili waweze kunufaika na SACCOS hii ambayo ina riba nafuu na kupata mkopo mkubwa ili waweze kutimiza malengo yao,"amesema Mbezi.

Kwa upande wake mwanachama Hassan Rashid amesema kuwa, chama hicho kimewasaidia sana hasa kwa upande wa faida kwani SACCOS imeleta fursa kwao ikiwa ni pamoja kutoa huduma za mikopo mbalimbali ambapo wengi wamewezeshwa kujenga nyumba za kisasa na mambo mengine ya maendeleo.
Amewataka watu kuchangamkia fursa ya kujiunga kwenye chama hicho ambacho kitakuwa kichocheo kutatua shida zao kuliko kwenda kukopa nje ambapo kuna riba kubwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news