Misimamo ya Mwenyekiti CCM Mara kwa chama, Serikali yampa heshima

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SAMUEL Kiboye maarufu kama Namba Tatu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara ametajwa kuwa kati ya viongozi wachache waliojipambanua katika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya uwazi na ukweli.
Hatua ambayo imetajwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa zilizomuwezesha kuyasoma makundi ambayo awali yalikuwa mwiba katika kukivuruga chama hicho mkoani Mara na hatimaye kuyavunja, hivyo kuwezesha ustawi bora wa chama.

"Mheshimiwa Kiboye ni miongoni mwa viongozi wachache ambao ni wabunifu sana, hatukutarajia kama angeweza kuyakomesha makundi sugu ambayo yalikuwa yamekomaa ndani ya chama, hivyo kusababisha chama mkoani hapa kuyumba, maana walitumia kila mbinu ikiwemo rasilimali fedha kuhakikisha kuwa, wanakuwa bega kwa bega na watu wao madarakani.

"Kiboye kwa sasa unaweza kumfananisha na hayati Ezekiel Mirumbe (mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Mara ambaye sasa ni marehemu, huyu mtu ni mchapa kazi na huwa hayumbishwi kuhusu jambo lolote linalohusu maslahi ya chama au Serikali.

"Mheshimiwa Kiboye ni miongoni mwa watendaji wachapa kazi sana, wawazi na wanaosimamia haki na ustawi bora wa CCM na Serikali mkoani Mara, hayumbishwi na mtu amekuwa mkweli na muwazi katika kukisemea chama na Serikali.

"Tunamuombea kwa Mungu azidi kuwa na afya njema ili azidi kukipigania chama, jambo la kujivunia sana ni pamoja na kufanikiwa kuyavunja makundi na kurejesha nidhamu ya hali ya juu,"amesema Mniko Mniko mkazi wa Mjini Musoma.

Aidha, Mniko ameungwa mkono na Martha Nyamonge mkazi wa mjini hapa ambapo amesema, Mheshimiwa Kiboye ni kiongozi mwenye hofu ya Mungu ambaye mara zote huwa anatekeleza majukumu yake kwa kumuomba Mungu amsimamie ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa haki na usawa.

Hayo wameyabainisha kwa nyakati tofauti ikiwa ni siku chache ambapo Mwenyekiti huyo aliwaonya viongozi ambao watajaribu kugusa fedha zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutambua kuwa, atakayefanya hivyo si tu jela inamuhusu bali atapoteza nafasi yake na atawajibishwa kwa haraka.

Katika ziara hiyo ambayo amekuwa akiifanya mara kwa mara kufuatilia namna ambavyo utekelezaji wa shughuli za maendeleo zinafanyika alisema, Serikali iliyopo madarakani inatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2021 ambayo imeainisha mambo mbalimbali kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania, hivyo akijitokeza yeyote mwenye nia ovu, mkono wa Serikali ni mrefu utamyakua popote alipo.

Pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye aliwataka wazabuni watakaopata tenda za kununua vifaa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,fedha iliyotolewa na Rais Samia Suluhu kutochelewesha vifaa kufika eneo husika.

Wito huo aliutoa wakati akikagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari ya Prof.Philemon Sarungi iliyopo wilayani Rorya wa Mara.

Post a Comment

0 Comments