Endasaki watajiwa faida za kuandika mirathi, wosia

NA MARY MARGWE

WANANCHI wametakiwa kuanza kuandaa utaratibu wa kuandika mirathi na kuacha wosia mapema kabla ya kutokea vifo ili kukabiliana na matatizo ya ukatili utakaoweza kujitokeza pindi kinapotokea kifo katika familia.
Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, Martha Sulle ameyasema hayo wakati alipokuwa akitoa mafunzo yahusuyo haki ya afya ya uzazi salama kwa wanawake na wasichana yaliyowezeshwa na Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Manyara(Manyara-Press Club-MNRPC) katika Kata ya Endasaki.

Sulle amesema, miongoni wa kundi linalofanyiwa ukatili zaidi ni wanawake mara wanaume zao wanapofariki na kuanza kudai haki yao ya mirathi ndio wanapoanza kukutana na matatizo makubwa na mazito kutoka kwa familia ya wanaume zao.

"Ni vema wananchi wakaanza kuandaa utaratibu wa kuandika mirathi na wosia kusaidia kurahisisha kazi wakati mtu anapokua amefariki, kwani wosia utakuwa umeainisha nini kipo na kimilikiwe na nani, na iwapo mali zitaongezeka wosia unarekebishwa tena ili kuongeza vilivyoongezeka na kuonyesha mmiliki wa hicho kilichopo,"amesema Afisa Ustawi wa Jamii huyo.

Aidha, amesema suala la kuandaa mirathi na wosia kwa wengi wao limekuwa ni tatizo huku wengi wao wakiamini kuwa kufanya hivyo ni kujiombea mkosi au kujihalalishia kifo, jambo ambalo lina msaada mkubwa hapo baadaye.

"Wanawake tuamke jamani, kama si kwa familia yenu basi hata kwa jirani yako uliwahi kusikia kama si kuona wanawake wanavyonyanyasika kudai mali wakati wa kutokea kwa vifo vya waume zao, hivyo ni vema mkalipa hilo kipaumbele zaidi hilo zaidi utasaidia kuwaongoza waliobakia kufuata wosia wa marehemu , badala wa ndugu baadaye kuanza kun'gan'gania mali za marehemu,"amesema.

Mbali na hilo pia aliwataka wazazi kuhakikisha wanapata nafasi ya kuwakagua watoto wao mara wanapowakogesha ili kujihakikishia kama wapo salama, kwani watoto wengi wamekuwa wakichezewa kwenye maungo yao, jambo ambalo ni ukatili kwa watoto.

Ameema, wazazi wengi wamekua mbali kabisa na watoto wao, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya watoto, kwani kuwakagua na kuwa nao karibu ni kulinda hali ya usalama wao.

Hata hivyo, wanawake na wasichana walielezwa mahali pa kwenda kushitaki kesi hizo za ukatili kama kwa balozi, mwenyekiti, kwa watendaji wa vitongozi, polisi na kwingineko.

Post a Comment

0 Comments