Mwalimu Nyerere ni Baba wa Taifa la Msumbiji-Balozi Mtumbuida

NA MWANDISHI MAALUM

Balozi wa Msumbiji nchini, Mhe Ricardo Mtumbuida amesema kuwa, Tanzania na Afrika ina wajibu mkubwa wa kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere kwa kuendeleza mshikamano wa kimataifa aliouasisi kipindi cha ukombozi wa Bara la Afrika.

Balozi Mtumbuida ameyasema hayo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Dar es Salaam alipotembelea onesho maalum linaloonesha kazi ya Baba wa Taifa Mwl J. K. Nyerere katika kuipatia Tanzania Uhuru na kusaidia ukombozi wa nchi zingine za Afrika ikiwemo Msumbiji.
Balozi wa Msumbiji nchini Mhe Ricardo Mtumbuida, wa pili kushoto akimsikiliza kwa makini Mhifadhi Mwandamizi wa Historia, Bi Flower Manase juu ya onesho la Mchango wa Mwalimu Julius K. Nyerere katika ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika, wa pili kulia ni Mkurugenzi Mkaazi wa UNESCO ofisi ya Dar es Salaam, Tirso Dos Santos, na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa Dkt Noel Lwoga.

“Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere si Baba wa Taifa la Tanzania pekee, ni Baba wa Taifa la Msumbiji pia, kazi yake katika ukombozi wa nchi yetu ni kubwa sana na ya kutukuka, ametupa heshima kubwa, tunajivunia uhuru tulio nao kwa sababu yake alituonesha njia na kushirikiana nasi kupata uhuru” anasema Balozi Mtumbuida

Balozi Mtumbuida aliyeambatana na Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO ofisi ya Dar ES Salaam, Bw. Tirso Dos Santos, licha ya kuupongeza uongozi wa Makumbusho ya Taifa kwa kuweka onesho maalum linaloelezea kazi ya Baba wa Taifa, amesama nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uhifadhi wa historia adhimu inayohusu nchi zote mbili (Tanzania na Msumbiji).
Balozi wa Msumbiji nchini Mhe Ricardo Mtumbuida, wa pili kulia akimsikiliza kwa makini Mhifadhi Mwandamizi wa Historia, Bi Flower Manase juu ya Pikipiki iyotumiwa na aliekuwa Rais wa Msumbiji Mhe Samora Machel katika harakati za ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika, kulia ni Mkurugenzi Mkaazi wa UNESCO ofisi ya Dar es Salaam, Tirso Dos Santos.

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt Noel Lwoga aliwashukuru Balozi Mtambuida na Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO ofisi ya Dar es Salaam Bw. Tirso Dos Santos kwa kuitembelea Makumbusho ya Taifa na kuongeza kuwa Taasisi yake imejipanga vizuri kuhakikisha uhifadhi wa Historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika unakuwa endelevu.

Mhe Balozi Mtambuida na Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO wapo kwenye ziara ya kutembelea vituo mbalimbali vilivyohifadhi historia ya Ukombozi wa Kusini wa Bara la Afrika chini ya uratibu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini.

Post a Comment

0 Comments