Mwinjilisti Temba:Watanzania njooni Hoteli ya Hyatt Regency leo muifahamu sarafu ya mauzo mtandaoni

NA GODFREY NNKO

MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba amewahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi leo Novemba 13, 2021 katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro iliyopo jijini Ilala, Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza Biashara ya Karne ya 21 ya Kidigitali kupitia mitandao kwa watu sahihi.

Temba ambaye ni miongoni mwa Watanzania ambao wamepewa karama ya kipekee katika kutabiri na kuombea pia ni kati ya wabobezi wazuri katika masuala ya uchumi huku akiwa na uzoefu mkubwa kutoka katika Mataifa 15 duniani.

Pia hivi karibuni Mwinjilisti Temba alikaribishwa na Mwenyekiti wa Chama cha United Party for National Development UPND Taifa, Stephen Katuka jijini Lusaka baada ya kutabiri juu ya ushindi wa UPND kilichomwingiza madarakani rais, Hakainde Hichilema ambao ulitimia kwa asilimia 100.

Ni katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Hichilima, hata hivyo baada ya hapo alikwenda kuishauri Serikali ya Botswana kupitia kwa Waziri anayehusika na Masuala ya Rais, Utumishi na Utawala wa Umma, Mheshimiwa Kabo Neale Sechele Morwaeng kuwa na maombi ya kitaifa na kuwafungulia Watswana waliokuwa wamefungiwa ndani baada ya takwimwu kuonyesha Botswana ilikuwa ikiongoza Duniani kwa maambukizi na vifo kutokana na ugonjwa wa UVIKO-19 na kufuatiwa na nchi ya India.

Baada ya ushauri wa Mwinjilisti Temba ndani ya wiki mbili Watswana walifunguliwa na maambukizi yakapungua kwa kasi sana baada ya serikali kutangaza maombi ya mwezi mmoja kutubu na kuomba Mungu aponye taifa.

Akizungumzia kuhusiana na biashara hiyo ya fedha kidigitali, Temba amesema kuwa, leo wataalamu wa Kimataifa watakuwepo katika kongamano hilo ili kuwapa fursa Watanzania kupata ufahamu sahihi.

"Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania kujitokeza kwa ajili ya kuwasikiliza wataalamu na shuhuda ndipo wafanye maamuzi, kwani Dunia sasa ipo katika mambo ya networking, hivyo hatuwezi kukwepa jambo hilo, bali kujifunza.
"Ushauri wangu kwa watanzania ni kwamba, ni vizuri tukapata elimu na shuhuda na hata kujaribu kwa maana hii biashara ya mitandao inasababisha mzunguko mkubwa wa fedha kupotea kwa jamii kwa njia ya fedha taslimu na kuwa katika mitandao kwa njia ya kidijitali,njia ambayo ni salama zaidi kuliko kuwa na fedha taslimu mkononi,"amesema.

"Nirejee tena wito wangu kwa Watanzania kuwa, mnakaribishwa kwenye networking ya biashara leo kuanzia saa tano asubuhi, Hyatty Regency Hotel, wavae nadhifu na waje kwa ajili ya kutengeneza fursa na vipato, kwa njia ya networking ambayo ni ya kimtandao,biashara ambayo inavuma sasa hivi Duniani, na Tanzania imeingia katika biashara hiyo, Watanzania wengi wanatengeneza fedha kwa njia ya mtandao, waje sasa wakutane na watu sahihi kutoka Afrika Kusini, ambao wapo nchini, wamekwenda pia Zanzibar na wamekutana hata na viongozi.

"Na sasa wapo Kilimanjaro hoteli, kwa hiyo leo kutakuwa na ufafanuzi mzuri kuhusiana na namna gani unaweza kupata kipato kupitia biashara ya networking ya kimtandao, ambayo inatokana na watu sahihi na kutakuwepo na shuhuda mbalimbali, ni vizuri watu kufika kwa sababu, kweli kumekuwa na biashara za kwenye networking ambazo nyingine zimekuwa si nzuri ni za kitapeli,lakini watu hao ni sahihi, chakula cha mchana kitakuwepo Kilimanjaro hoteli, wote ambao wanataka kufanya biashara za kisasa zaidi na biashara ambazo wanaweza kutengeneza fedha nyingi kwa wakati mfupi waweze kufika katika hoteli ya Kimataifa ya Kilimanjaro.

"Watanzania wote ambao wanaotaka kutengeneza vipato kwa njia zuri na salama, hii ni nafasi yao kuja kupata maarifa na kueleweshwa zaidi katika hoteli ya Kilimanjaro,"amesema

TANZANIA INAELEKEA HUKO

Wito huo unakuja ikiwa Juni 13, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa Taifa kujiandaa kutumia sarafu za mauzo ya mtandaoni maarufu kama Bitcoin.

"Najua nchi nyingi duniani hazijaanza kutumia sarafu za mauzo ya mtandaoni. Hata hivyo, natoa wito kwa Benki ya Kuu ya Tanzania kuanza kufuatilia yanayojiri na kujiandaa;

Hotuba Rais Samia huko jijini Mwanza siku hiyo ilifuata baada ya nchi ya El Salvador kutangaza kupitisha Bitcoin kama njia halali ya malipo ya zabuni sambamba na mataifa mengine ya Amerika Kusini na Kati kuonyesha utayari wao wa kutumia sarafu hiyo.

Mheshimiwa Rais alisema, Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuanza maandalizi muhimu ya mabadiliko ya hatua katika mtazamo wa ulimwengu juu ya benki, ikichagua sarafu za mtandaoni kama mustakabali wa fedha.

“Tumeshuhudia kuibuka kwa safari mpya kupitia mtandao.Najua kuwa mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania hawajakubali au kuanza kutumia njia hizi. Lakini wito wangu kwa Benki Kuu ni kwamba mnatakiwa kuanza kufanyia kazi maendeleo hayo. Benki Kuu inapaswa kuwa tayari kwa mabadiliko na sio kukutwa hamjajiandaa,”amesema.

Aidha, kauli hiyo ya Rais Samia imekuja sambamba na maoni ya hivi karibuni kutoka kwa Elon Musk ambaye amekuwa mshawishi mkubwa wa bei ya Bitcoin tangu kuanzishwa kwake zaidi ya mwongo mmoja uliopita.

Hivi karibuni, kiongozi huyo wa Tesla amesema, kampuni yake ya magari ya umeme itakubali Bitcoin kama njia ya malipo.

ZANZIBAR NAPO

Wakati huo huo, Novemba 8, 2021 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mheshimiwa Mudrick Ramadhan Soranga alisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakaa pamoja na wadau wa sarafu ya kidigitali (digital currency) ili kuona ni kwa namna gani Zanzibar itaweza kuitumia sarafu hiyo.

Mheshimiwa Saranga ameyasema hayo ofisini kwake Mwanakwerekwe iliyopo Wilaya ya Magharibi B mjini Unguja wakati alipokutana na viongozi wa Kampuni ya Hypertech Company Limited kutoka nchini Afrika Kusini ili kujadili namna ya kuitambulisha sarafu ya kidigitali kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akiwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri namna Dunia inavyotumia sarafu hiyo, mwakilishi wa biashara hiyo kutoka kampuni ya Hypertech Company, ndugu Joe Chuene amesema kuwa, mwelekeo wa Dunia kwa sasa ni kutumia sarafu ya kidigitali kufanya manunuzi ya vitu mbalimbali na kusema kuwa, sarafu hiyo inatumiwa na watu wengi pamoja na makampuni makubwa kote duniani.

Pia aliongeza kuwa, kwa sasa mzunguko wa sarafu ya kidigitali umefikia kiwango cha dola za kimarekani trilioni 3.2 duniani kote, hivyo kuiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuitambulisha sarafu hiyo ili iweze kutumika kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi na Serikali kwa ujumla.

Akifunga mjadala huo, Mheshimiwa Waziri Saranga aliwahakikishia viongozi hao kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar italichukulia sula hilo kwa umuhimu mkubwa ili kuona jinsi gani jambo hilo linaweza kufanikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news