Waziri Mkuu:Wakuu wa mikoa msiwazuie wananchi kuingiza mbolea nchini

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa hasa ya mipakani kutozuia wananchi kuingiza mbolea kutoka nje ya nchi na vilevile kutoruhusu utoaji wa mbolea kutoka ndani kwenda nje ya nchi ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mbolea.
Ametoa agizo hilo leo Novemba 12, 2021 wakati akiahirisha Mkutano wa tano wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma. “Matumizi ya mbolea, mbegu bora na viuatilifu ni muhimu katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.”

“Upatikanaji wa mbolea duniani kote umeathiriwa na uwepo wa UVIKO 19, hivyo kusababisha kusimama kwa uzalishaji, baadhi ya nchi kusitisha uuzaji wa mbolea nje, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na upungufu wa malighafi za kutengeneza mbolea kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka yake na hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji na bei ya mbolea.”

Waziri Mkuu amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa katika kuhakikisha pembejeo za kilimo hususan mbolea zinapatikana kwa bei nafuu, kwa wakati na kiwango cha kutosha. “Miongoni mwa hatua hizo ni matumizi ya mifumo ya upatikanaji wa mbolea kupitia uzalishaji ndani ya nchi na uagizaji wa mbolea kwa pamoja kutoka nje ya nchi.”

Ametaja baadhi ya hatua za haraka ambazo Serikali imechukua katika kukabiliana na hali hiyo kuwa ni pamoja na kuwasiliana moja kwa moja na wazalishaji wa mbolea katika nchi rafiki ili kupata mbolea kwa gharama nafuu na kuruhusu wafanyabiashara kuingiza mbolea nchini bila kutumia zabuni za mfumo wa ununuzi wa pamoja na kuuza kwa bei ya ushindani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema hatua hiyo imesaidia kuongeza kiwango cha mbolea kilichoingizwa nchini kati ya Julai na Oktoba 2021. “Katika kipindi hicho, tani 48,400 za mbolea ya urea ziliingizwa nchini ikilinganishwa na tani 33,948 kwa zabuni ya mfumo wa pamoja msimu wa 2020/2021.”

“Hatua nyingine ni kuhamasisha matumizi ya mbolea mbadala wa DAP na Urea kama vile NPK, NPS, NPSZinc, Nafaka ya Minjingu, mbolea za asili, chokaa na mbolea ya Fomi Imbura inayozalishwa na Kiwanda cha Fomi cha Burundi na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya ndani vya kuzalisha mbolea ikiwa ni sehemu ya suluhisho la muda mrefu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema tayari ujenzi wa kiwanda cha Kampuni ya Itracom Fertilizers Limited kutoka Burundi umeanza na utakapokamilika kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka. Kadhalika, kuongeza uzalishaji katika kiwanda cha Minjingu ili kizalishe sawa na uwezo wake wa tani 100,000 kwa mwaka.

Amesema Serikali inaendelea kukamilisha mazungumzo na Serikali ya Burundi kuhusu kununua mbolea ya Fomi Imbura, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuzitumia aina nyingine za mbolea kwani zinatumika kwa mafanikio kwa nchi jirani na baadhi ya maeneo ya Tanzania.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) imekwishaagiza tani 20,000 za mbolea ya kupandia (DAP) na tani 60,000 za mbolea ya kukuzia (Urea) na mbolea hiyo itauzwa kwa gharama nafuu ambayo inalingana na uwezo wa wakulima wetu nchini.

Amesema hatua nyingine ni ukamilishaji wa utafiti wa afya ya udongo katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Mtwara, Lindi, Tanga, Ruvuma, Tabora na Kigoma kwa lengo la kuwezesha viwanda vya mbolea hususan vilivyoko nchini kuzalisha mbolea kulingana na afya ya udongo sambamba na matumizi sahihi ya mbolea.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news