Mzee Nanyaro ajenga kaburi barabarani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MWANAKIJIJI wa Kijiji cha King’ori wilayani Arumeru mkoani Arusha,John Nanyaro ameingia katika mgogoro na wananchi baada ya kufunga barabara kwa kujenga kaburi akidai eneo hilo ni mali yake.
Matukio ya namna hii yamekuwa yakitokea mara chache Duniani huku yakihusishwa na imani za kishirikina na wakati mwingine migogoro ya ardhi.Ni hivi karibuni ilizuka mijadala mikali katika mitandao ya kijamii ikielezea kuhusiana na kisa cha kushangaza cha kukutwa kaburi hili pichani katikati ya barabara iliyopo mjini Cherkisla katika Jimbo la Silvas jijini Ankara nchini Uturuki, kaburi hilo hadi leo halijulikani aliyezikwa humo wala sababu ya kufanya hivyo. (Picha na theAZB).

Kwa nyakati tofauti wakazi wa kijiji hicho wakiwemo ndugu wa mlalamikiwa wamesema, barabara aliyofunga mwanakijiji huyo imekuwa ikitumiwa tangu mwaka 1991.

Aidha, kwa mujibu wa Joel Nanyaro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano ya Kijiji cha King'ori amesema wanapinga uamuzi ya ndugu yake, John kufunga barabara hiyo.

“Huyu ni ndugu yangu, anachokifanya ni kuvunja sheria na kutaka kupora ardhi hiyo ambayo yeye mwenyewe aliuza eneo hilo kwa marehemu Wilfred Urio,” amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha,mtoto wa marehemu Wilfred, Amani Urio amesema, ameshangazwa na Mzee Nanyaro kumfungia barabara ya kwenda kwake na kujenga kaburi bandia usiku na sasa amekuwa akimtisha kuwa atampoteza.

Amani Urio amesema, aliamua kulifikisha suala hilo katika Mahakama ya Mwanzo King’ori ambako hakimu alitoa hukumu kuwa kesi hiyo ipelekwe Baraza la Ardhi Novemba 5,mwaka huu.

“Nimeshangazwa na uamuzi wa hakimu ambao nadhani una shinikizo la ninaowalalamikia kufunga barabara, kwani viongozi wote wa kijiji walitoa ushahidi kuthibitisha Mzee John kuvamia barabara,” alidai Amani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha King’ori, Elipokea Nanyaro amesema yeye na viongozi wenzake wanatambua Mzee John amevamia eneo la barabara.

“Tulitoa ushahidi lile lilikuwa eneo la barabara tangu mwaka 1991 na lilitolewa kwa kufuata taratibu zote,” amesema.

Mzee wa ukoo wa Nanyaro, Cleopa Nanyaro pia amesema, suala hilo lilishafikishwa katika kikao cha familia na Mzee John alitakiwa kurejesha ardhi anayoing’ang’ania.

Mzee John Nanyaro mwenyewe amesema, eneo la barabara ni mali yake na amejenga kaburi la kijana wake.

“Mimi sijavamia eneo, hapa ni mali yangu hakuna barabara,” alidai.

Hakimu wa Mahakama ya mwanzo King’ori, Prince Gedion amesema, tayari ameshapeleka jambo hilo Baraza la Ardhi kwani linahusisha masuala ya ardhi.

Pia amesema, awali Katibu Tarafa alifika ofisini kwake kulifuatilia suala hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news