NHC yatakiwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuendelea kuwekeza miradi ya kimkakati itakayoliwezesha shirika kujiongezea kipato.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia sehemu ya Jengo la Kibiashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mutukula wilayani Misenyi mkoani Kagera alipokwenda kukagua mradi wa jengo hilo tarehe 23 Novemba 2021. (PICHA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM).

Dkt.Mabula ametoa kauli hiyo Novemba 23,2021 wakati akikagua mradi wa jengo la kibiashara la NHC lilipo mpakani mwa Tanzania na Uganda eneo la Mutukula wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.

Naibu Waziri ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili mkoani Kagera alisema, ilichofanya NHC kujenga jengo la kibiashara katika mpaka wa Tanzania na Uganda Mutukula ndicho serikali inachokitaka pale inapokuwa na taasisi zinazojitegemea katika uendeshaji pia ziwe na njia tofauti za kujiongezea kipato kitakachosaidia kuongeza miradi mingine.

"Hiki ambacho NHC mmekifanya hapa kujenga jengo la biashara Mutukula ndicho inachokitaka serikali kuwa inapokuwa na taasisi inayojitegemea kiuendeshaji pia iwe na njia tofauti za kujiongezea kipato cha shirika,"amesema Dkt.Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera Maneno Mahenge (Kulia) alipokwenda kukagua Jengo la Kibiashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Mutukula wilayani Misenyi mkoani Kagera tarehe 23 Novemba 2021. (PICHA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM).

Kwa mujibu wa Dkt Mabuka, mradi wa jengo la biashara Mutukula unatoa fursa kwa wafanyabiashra kutoka nchi jirani ya Uganda kuja Tanzania kununua bidhaa kwani awali ilikuwa aibu kuona wafanyabiashara wakienda kununua bidhaa katika maduka ya nchi hiyo.

"Ilikuwa aibu tunaenda upande wa pili kununua bidhaa lakini sasa na wao waje hapa kufanya biashara na hii ni alama tosha kuwa tunaanza kubadilika,"amesema Naibu Waziri Mabula.

Aidha, Dkt.Mabula aliongeza kuwa, ana imani mradi wa jengo la kibiashara Mutukula ukienda vizuri eneo lingine linalokusudiwa kujenga maduka litapata msaada wa fedha za ndani zitakazopatikana kupitia mradi huo.

Naibu Waziri Mabula aliongeza kuwa, ni kweli wafanyabiashara wadogo wamachinga hawawezi kupanga katika jengo la mradi huo lakini shirika linaweza kujenga maduka kuzunguka jengo hilo yanayoweza kubadilisha sura ya eneo kuonesha kuwa eneo hilo limepangwa na isiwe viduka visivyoonesha tofauti kati ya eneo lilipangwa na lisilopangwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifurahia bidhaa aliyonunua kwenye moja ya maduka yaliyopanga katika jengo la Kibiashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mutukula wilayani Misenyi mkoani Kagera alipokwenda kukagua mradi wa jengo hilo tarehe 23 Novemba 2021.(PICHA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM). 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Projestus Tegamaisho Mutukula amelishukuru Shirika la Nyumba la Taifa kwa uamuzi wake wa kuwekeza mradi huo katika eneo la Mutukula ambapo aliiomba NHC kuangalia uwezekano wa kuwekeza mradi kama huo katika mji unaopanuka wa Bunazi wilayani Misenyi.

"Niwashukuru NHC kwa kutuwekea kitega uchumi cha jengo hili na tunaomba mtujengee jengo lingine katika mji wa Bunazi ili maeneo ya Misenyi yawe na uwelezaji mkubwa,"amesema Tegamaisho.

Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera Maneno Mahenge alisema, mradi wa jengo la Mutukula kwa sasa umefikia asilimia 99 na mradi huo umetumia asilimia 50 tu ya eneo lake lenye ukubwa wa mita za mraba 7900.
Sehemu ya ndani ya Jengo la Kibiashara la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo Mutukula wilayani Misenyi mkoa wa Kagera. (PICHA NA MUNIR SHEMWETA-WANMM).

"Tunataka mradi huu wa kitega uchumi hapa Mutukula uwe shopping centre area inayotembelewa na wananchi wengi wakiwemo wa nchi jirani ya Uganda na jengo hili tayari lina wapangaji 36,"amesema Mahenge.

Aidha, katika kuhakikisha NHC unawekeza majengo ya kimkakati maeneo ya mipakani Meneja huyo wa Shirika la Nyumba la Taifa mkoa wa Kagera alieleza kuwa, tayari amepeleka Andiko Makao Makuu ya NHC kwa ajili ya kuanzisha miradi kama wa Mutukula katika eneo la Rusumo mpaka wa Tanzania na Rwanda pamoja na Kabanga katika mpaka wa Tanzania na Burundi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news