Rais Dkt.Mwinyi ataja faida ya tasnia ya ukadiriaji majenzi nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dokta Hussein Ali Mwinyi, amesema sekta ya ukadiriaji majenzi ni taaluma na fani muhimu katika kufanikisha maendeleo ya nchi na ujenzi wa uchumi wa taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Dokta Mwinyi ameyasema hayo Novemba 12, 2021 katika hafla ya uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wakadiriaji Majenzi Tanzania (TIQS), uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mazizini nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Dokta Mwinyi aliyewakilishwa katika hafla hiyo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema taaluma ya ukadiriaji majenzi (quantitity survey) ni muhimu sana pale inapotumika katika kufanikisha miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu kwa ufanisi.

Akiongelea dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar kuzingatia ipasavyo mchango wa wataalamu wa ukadiriaji majenzi ili kuhamasisha ujenzi imara wa uchumi wa buluu, Rais Dokta Mwinyi amesema, “sisi kama Serikali tutajitahidi kuwatumia na pia kuhamasisha wawekezaji watumie taaluma zenu katika kuwekeza na kutekeleza miradi yao ya ujenzi”.

Naye, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Bi Riziki Pembe Juma amesema serikali inatambua umuhimu wa tasnia ya ukadiriaji majenzi kama sehemu ya njia bora ya kufanikisha mipango ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi hii.

Akibainisha fursa mbalimbali za kufanikisha maendeleo zilizopo na zinazoendelea kujitokeza nchini, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Bw. Sharif Ali Sharif, amewahamasisha wataalamu wakadiriaji majenzi (quantity surveyors), kujiandaa vyema kuitumia taaluma yao katika kufanikisha miradi ikiwemo ya ujenzi wa bandari, barabara na mahoteli, ili kusaidia juhudi za kuijenga nchi kiuchumi.

Akiwakaribisha pia washiriki wa Kongamano la Wakadiriaji Majenzi wa Afrika Mashariki walioshiriki katika Mkutano huo, Rais wa TIQS Tanzania, Dkt Bernard Ndakidemi amebainisha azma ya taasisi yake kuchangamkia fursa na kuhamasisha wawekezaji mbali mbali kuja kuwekeza katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Viongozi mbali mbali wa Serikali na wanasiasa wamejumuika katika Mkutano huo, ambao ni pamoja na Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Wahandisi, Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Dkt Abdalla Juma Abdalla Mabodi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news