TAKUKURU yatega mtego kwa watakatishaji fedha

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

FRIDA Wekesi ambaye ni Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kilimanjaro amewataka watumishi wa umma wakiwemo viongozi wa Serikali za mikaa mkoani hapa kuacha mara moja kutumika kama daraja la kupitishia fedha zisizo halali katika akaunti zao za benki, kwani watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema, taasisi hiyo inafuatilia kwa karibu mienendo ya baadhi ya watendaji mkoani hapa, hivyo imewataka kuwa makini na fedha zinazopitishwa kwenye akaunti zao huku wakizitumia kwa shughuli zao binafsi.

Wekesi ameyasema hayo wakati akiwasilisha mada katika semina ilijumuisha viongozi wa vijiji na kata katika Jimbo la Same Magharibi ambayo iliangazia kuhusu umuhimu wa uaminifu na athari za rushwa kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi za shina na kata.

Mkuu huyo amesema, makosa ya kutumiwa fedha zisizojulikana chanzo halali cha mapato yake na kuzitumia katika shughuli halali yanaangukia katika makosa ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana, hivyo watapoteza kazi zao.

"Usifikiri unapotumiwa fedha zisizohalali na kuzitumia kujenga nyumba, kununua vitu vya thamani yakiwemo magari, kulipa ada za watoto shule kunaleta uhalali wa zile fedha la hasha, ikitokea ukafanya hivyo ni kinyume na sheria, epukeni huo mtego,"alionya Mkuu huyo.

Pia amesema, fedha zozote zinazotumwa kwenye akanti za fedha zinapaswa kuwa na maelezo ya kutosheleza ikiwemo ushahidi wa maelezo hayo, kwani zitakapobainika kutokuwa halali utaunganishwa katika makosa ya utakatishaji fedha mpaka itakapothibitika vinginevyo.

"Kutokujua sheria sio kinga, mnapaswa kujiridhisha na fedha zote zinazotumwa kwenu kabla ya kuzitumia maana tukikukamata na rushwa ama utakatishaji fedha hatutaangalia kama wewe ni kiongozi, mtumishi mwenzetu ama la, tutaangalia kama unahusika kwenye kosa tu,"ameongeza.

Wekesi pia alitaka viongozi hao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutochagua viongozi wa ngazi mbalimbali kwa misingi ya rushwa, kwani hawatapata maendeleo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Uhamiaji mkoani Kilimanjaro, Martin Mwenda alitaka viongozi wa ngazi mbalimbali kufanya utambuzi wa wageni wote wanaohamia katika maeneo yao kwani kazi kubwa ya kwanza ni ulinzi katika makazi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news