Rais Dkt.Mwinyi ataja faida za matumizi sahihi ya Bahari

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba iwapo bahari itatumika ipasavyo, hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza dhana ya uchumi wa Buluu ambayo inahusisha matumizi endelevu ya bahari.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na Uongozi wa Maskani Kachorora (CCM) baada ya mazungumzo na uongozi huo alipokutana nao katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Maskani ya Kachorora, ambao ulifika Ikulu kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kutekeleza vyema majukumu aliyopewa na wananchi ndani ya mwaka mmoja tokea apate wadhifa wa Urais.

Sambamba na kutekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Rais Dkt.Mwinyi amesema kuwa, Serikali anayoiongoza ya Awamu ya Nane imeamua kwa makusudi kutekeleza Dira ya Uchumi wa Buluu kwa kutambua umuhimu wake katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo pamoja na kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Alieleza kwamba, miongoni mwa sekta ambazo zimepewa kipaumbele katika dira hiyo ni sekta ya uvuvi ambao lengo kubwa ni kuhakikisha sekta hiyo inaimarishwa ili iweze kuleta tija kwa wavuvi wenyewe pamoja na nchi kwa ujumla ambapo serikali itahakikisha inawawekea mazingira mazuri wavuvi ikiwa ni pamoja na kuwapatia zana za kisasa na elimu inayohusiana na sekta hiyo.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kwamba maendeleo makubwa yataendelea kupatikana Zanzibar iwapo amani, utulivu na ushirikiano vyote kwa pamoja vitaendelea kudumishwa huku akitumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Maskani hiyo kwa kuthamini na kuzipongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza. 

Pia Rais Dkt.Mwinyi aliunga mkono wazo la uongozi huo la kufufua mashindano ya Ligi ya Muungano ambayo alisema yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza soka la Zanzibar.

Katika hatua hiyo, Rais Dkt.Mwinyi alitilia mkazo na kueleza hatua za makusudi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali anayoiongoza kupitia wizara husika katika kuhakikisha Ligi Kuu ya Zanzibar inapata udhamini ikiwa ni pamoja na kufanya harambee iliyokusanya fedha za kutosha kwa ajili ya kuiunga mkono Ligi ya Zanzibar.

Mapema uongozi huo wa Maskani ya Kachorora yenye makazi yao jijini Zanzibar ulimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kutekeleza vyema majukumu yake ambayo ndani ya mwaka mmoja wa uongozi wake wananchi wameweza kufarijika na kuonesha matumaini yao makubwa waliyokuwa nayo kwa kiongozi huyo.

Uongozi huo pia ulimpongeza Rais Dkt.Mwinyi kwa kutekeleza zana na Dira ya Uchumi wa Buluu ambao walieleza iwapo utatekelezwa ipasavyo mafanikio makubwa yatapatikana katika sekta ambali mbali zinazohusiana na uchumi huo ikiwemo sekta ya uvuvi.

Aidha, uongozi huo ulieleza haja ya kuwepo kwa namna bora ya uvuvi ili kuweza kuhifadhi mazingira pamoja na kulinda viumbe vya bahari.

Sambamba na hayo, uongozi huo wa Maskani ya Kachorora ulieleza haja ya kufufuliwa kwa mashindano ya Ligi ya Muungano ambapo walieleza kwamba mashindano hayo yanazisaidia timu za Zanzibar kuweza kushiriki katika ligi za Kimataifa sambamba na kuweza kupata kipato kwa timu shiriki.

Katika hatua nyingine, uongozi huo wa Maskani ya Kachorora umeahidi kuendelea kushirikiana na Rais Dkt.Mwinyi sambamba na kuendelea kumuunga mkono katika uongozi wake uliotukuka kwani wameanza kuona mwanga wa matumaini ya Zanzibar kuzidi kupata maendeleo endelevu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news