Rais Samia kupitia TASAF awapa tabasamu wanakijiji

NA JAMES K.MWANAMYOTO

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za ujenzi wa daraja lingine katika Kijiji cha Laja kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Laja wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Mhe. Chaurembo ametoa pongezi hizo baada ya kamati yake kumuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuhakikisha TASAF inajenga daraja hilo ili kutatua changamoto iliyokuwa ni kikwazo kikubwa cha upatikanaji wa huduma za kijamii.

Mhe. Chaurembo amefurahishwa na kitendo cha Mhe. Mchengerwa kuomba ridhaa ya Mhe. Rais kutoa fedha za TASAF ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya kamati yake yaliyolenga kutatua changamoto za wananchi wa eneo hilo.

Ameongeza kuwa, kwa kawaida kamati yake inapofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi, inakuwa imejiwekea lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, hivyo uamuzi wa Mhe. Rais, umewezesha azma ya kamati yake.
Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Laja wakimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Laja wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Awali, Mhe. Mchengerwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo na ndio maana amechukua hatua madhubuti ya kuwajengea daraja ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za kijamii.

Amesema pamoja na kukamilisha ujenzi wa daraja linalounganisha Vijiji vya Laja na Umbang’w, Mhe. Rais kupitia TASAF ameahidi kujenga daraja lingine katika korongo lililoko karibu na shule ya Msingi Laja kwani wakati wa masika watoto wa shule walioko ng’ambo ya korongo wanashindwa kuhudhuria masomo.

“Mhe. Rais ameniagiza niwaambie kwamba, amekubali ombi lenu la kuwajengea daraja lingine ili wanafunzi waweze kushiriki masomo kikamilifu na wakazi wa eneo hili washiriki shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Katika kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais, Mhe. Mchengerwa amewaagiza watendaji wa TASAF kufanya tathmini ya gharama za ujenzi wa daraja hilo mapema iwezekananvyo ili ujenzi uanze mapema.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akipokea risala ya utekelezaji wa miradi ya TASAF toka kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Laja, Bw. Daniel Mpigachai wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo akijadiliana jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Laja, Bibi Balbina Sulle akitoa ushuhuda kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wa namna TASAF ilivyowanufaisha kwa kuwajengea daraja ambalo limeweza kutatua changamoto za miundombinu zilizokuwa zikiwakabili wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka wananchi wa eneo hilo wakutane kwa ajili ya kufanya vikao vya tathmini ya miradi ambayo itaingia katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Nne ambayo tayari Mhe. Rais ameshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.

“Viongozi wa kuteuliwa na Viongozi wa kuchaguliwa tujiongeze kwa kuwatumia wadau wa maendeleo kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yenu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, kila kiongozi akitumia nafasi yake vizuri ya kuwahudumia wananchi kwa kutambua dhamana aliyo nayo kuwa ni ya kuwahudumia wananchi, hakika taifa linaweza kumaliza changamoto kwa wakati.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Abdallah Chaurembo na Wajumbe wa kamati yake wakikagua daraja lililojengwa kwa kutumia fedha za TASAF katika Kijiji cha Laja wakati wa ziara ya kikazi ya kamati yake iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Akitoa ushuhuda wa namna TASAF ilivyowasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma za kijamii katika eneo hilo, mkazi wa Kijiji cha Laja, Bibi Balbina Sulle ameipongeza TASAF kwa kuwajengea daraja imara ambalo limerahisisha upatikanaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto na ya elimu kwani sasa hivi wanafunzi wamekuwa wakishiriki masomo bila kikwazo cha kivuko.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Halmshauri ya Wilaya ya Arusha na Karatu.

Post a Comment

0 Comments