RC Malima atembelea vituo vya afya Korogwe

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Adam Malima akiambatana pamoja na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhe. Kalist Lazaro Bukhay ametembelea miradi ya ujenzi wa Vituo vya Afya katika Wilaya ya Korogwe. 

Miradi hiyo ya ujenzi wa Vituo vya Afya inajumuisha Kituo cha Afya cha Mgombezi na Kituo cha Afya cha Kwamsisi vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe pamoja na Kituo cha Afya cha Mnyuzi kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. 

Ziara hiyo ya kutembelea miradi ya ujenzi wa Vituo vya Afya imefanyika Novemba 15, mwaka huu.
Kupita fedha za makato ya tozo ya miamala ya simu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipatia Wilaya ya Korogwe kiasi cha Shilingi Milioni 750 za awali kwaajili ya utekelezaji wa ujenzi wa Vituo vitatu vya Afya ambavyo ni Mgombezi, Kwamsisi pamoja na Mnyuzi ikiwa kila kituo kimepatiwa kiasi cha Shilingi Milioni 250.

Baada ya utekelezaji wa ujenzi wa majengo ya awali katika Kituo cha afya Mgombezi, Kwamsisi pamoja na Mnyuzi kukamilika, Serikali itaongeza fedha nyingine kiasi cha Shilingi Milioni 750 ili kukamilisha ujenzi wote wa vituo vyote vitatu katika Wilaya ya Korogwe ikiwa kila kila Kituo cha Afya ujenzi wake utagharimu kiasi cha Shilingi Milioni 500.

“Muwe na uchungu na mradi huu kama mali za familia zenu” alisema Mhe. Adam Malima ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga wakati wa ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa Vituo vya Afya katika Wilaya ya Korogwe. Mhe. Malima alisisitiza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili za Wilaya ya Korogwe wakamilishe miradi hiyo ya vituo vya afya kwa wakati ili iweze kuwahudumia Wananchi.

Katika hatua nyingine Mhe. Malima amemuagiza Kaimu Mkuu wa Wilaya Korogwe Mhe. Kalist Lazaro Bukhay pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili za Wilaya hiyo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa Vituo vyote vya afya ifikapo Januari 2022. 

Mhe Malima alisisitiza kuwa fedha zote za miradi zimeshaingizwa katika Halmashauri hivyo hakuna sababu ya msingi itakayosababisha uhaba wa vifaa vya ujenzi kwajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa maelekezo yote uliyotoa tumeyapokea na tutayafanyia kazi” alisema Mhe. 

Kalist Lazaro Bukhay ambaye ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Korogwe wakati wa ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa Vituo vya Afya. 

Mhe. Bukhay alifafanua kuwa yeye pamoja na viongozi kutoka Halmashauri zote mbili za Wilaya ya Korogwe watahakikisha wanafanya kazi kwa bidi ili itakapofikia Januari 2022 ujenzi wa vituo vyote vitatu vya afya uwe umekamilika.

Kwaupande mwengine, Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ambao ni wanufaika wa miradi ya ujenzi wa Vituo cha Afya walitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha kwaajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya.

Post a Comment

0 Comments