Sekondari ya Anna Abdallah ya mjini Masasi yapongezwa

NA FRED KIBANO

SERIKALI imepongeza ujenzi wa shule ya sekondari Anna Abdallah unaoendelea katika Halmashauri ya Mji Masasi wa vyumba vinne vya madarasa ambavyo vitatumika kwa ajili ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mapema mwaka 2022.
Akiongea baada ya ukaguzi huo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema matarajio ya Serikali ni kuwa ifikapo Desemba 15, mwaka huu ni lazima madarasa yote yawe yamekamilika na kuwa tayari kwa matumizi kwani hakutakuwa na chaguo la pili hapo mwakani kama ilivyozoeleka.

“Kwanza niwapongeze kazi inaonekana, viwango vyenu vya ujenzi wa madarasa Halmashauri ya Mji Masasi mmefanya vizuri na mpaka Desemba 15 mtakuwa mmemaliza, nisisitize sasa mnapokwenda kukamilisha kazi hii tuendelee kuzingatia thamani ya fedha na viwango vionekane,”amesema.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Masasi, Elias Mtirungwa amesema halmashauri yake inatekeleza mpango wa maendeleo ya ustawi wa jamii na mapambano ya UVIKO-19 ambapo alipokea kiasi cha shilingi milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 35 vya madarasa kwenye shule 9, milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum Masasi, milioni 440 kwa ajili ya vyumba viwili vya madarasa kwenye shule shikizi ya Mkajamila ambapo utekelezaji wake unaendelea vizuri.

“Utelekelezaji wake na hali ilivyo hadi kufikia sasa, ni kuwa madarasa 21 yapo katika hatua ya upauaji, madarasa 16 yapo katika hatua ya umaliziaji, bweni la wanafunzi lipo katika hatua ya msingi na matarajio ni kukabidhi madarasa ifikapo Desemba 12, 2021,”amesema.

Akisoma taarifa ya Shule ya Sekondari Anna Abdalla, Mkuu wa shule hiyo, Emanuel Kabale amesema shule yake ilipokea kiasi cha shilingi milioni 80 kwa ajili ya kujenga vyumba vinne vya madarasa na hatua waliyofikia ni hatua ya upauaji na wanatarajia kukabidhi mradi mapema Desemba 8, mwaka huu.

Aidha, amesema fedha iliyotumika mpaka sasa ni shilingi 70,917,736.44 na fedha kiasi cha shilingi 9,082,263.56 ni kwa ajili ya kazi ndogondogo zilizobaki na samani za madarasa zimekwishanunuliwa.

“Tunahitaji kupata madarasa manne yenye viti na meza hamsini kwa kila darasa na hivyo kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa, viti na meza kwa wanafunzi,"amesema.

Post a Comment

0 Comments