Serikali yaanza mchakato wa kuufanyia ukarabati mkubwa Uwanja wa Ndege Moshi

NA MWANDISHI MAALUM

IMEELEZWA kuwa katika kuhakikisha huduma za utalii na usafiri wa anga zinaimarika katika Mkoa wa Kilimanjaro, Serikali itakifanyia ukarabati mkubwa uwanja wa ndege wa Moshi ( Moshi Aerodrome & King George VI Playing Field).
Muonekano wa uwanja wa ndege wa Moshi ambao ulijengwa mwaka 1954, na unatarajiwa utafanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni.

Hayo yamesemwa Novemba 21, 2021 na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokagua uwanja huo na kusisitiza kuwa tayari kiasi cha shilingi bilioni kumi zimetengwa kwa ajili ya kuuboresha kwa awamu ya kwanza.

Amewataka wadau wa utalii mkoani Kilimanjaro kuweka mazingira bora ya kukuza utalii wa mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kwa kutumia uwanja huo kikamilifu.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,Mhandisi Godfrey Kasekenya akisisitiza jambo kwa Mbunge wa Moshi Mjini, Mhe. Priscus Tarimo alipokagua uwanja wa ndege wa Moshi ambao utafanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni (kulia), ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Motta Kyando na Kaimu Meneja wa uwanja huo, Mhandisi Dickson Mmbando wa pili kulia. (Picha zote na WUU).

Naibu Waziri huyo ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha mkandarasi wa uwanja huo anapatikana kwa haraka na kuitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), kuboresha huduma katika uwanja huo ili kuvutia wadau wengi kutumia.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro, Mahndisi Motta Kyando amesema ukarabati wa uwanja huo utahusisha urefushaji wa njia ya kutua na kuruka ndege ambayo itajengwa kufikia urefu wa mita 1,300 kwa kiwango cha lami, ujenzi wa uzio na barabara za kuzunguka uwanja huo na barabara ya maingilio ya kwenda katika uwanja huo.

Amesisitiza kuwa, maandalizi yote yako katika hatua za mwisho,hivyo amewataka watakaopata fursa katika ukarabati huo kufanya kazi kwa uzalendo.
Naye Mbunge wa Moshi Mjini, Mhe. Priscus Tarimo ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuukarabati uwanja huo na kusisitiza kuwa ukarabati huo utaboresha biashara na utalii katika mkoa wa Kilimanjaro na kukuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kaimu Meneja wa uwanja huo, Mhandisi Dickson Mmbando amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa uwanja huo ukikarabatiwa utavutia wasafirishaji wengi wa anga kuutumia na kuongeza tija kwa wananchi.
Uwanja huo wa ndege Moshi ni miongoni mwa viwanja 59 vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), na miongoni mwa viwanja vikongwe hapa nchini ambao ulifunguliwa mwaka 1954 ukijulikana kama Moshi Aerodrome & King George VI Playing Field.

Post a Comment

0 Comments