Serikali yasisitiza itaendelea kuajiri walimu kukabiliana na uhaba

NA FRED KIBANO

SERIKALI imesema inaendelea kupunguza uhaba wa walimu katika shule zake ili kukabiliana na upungufu wa watumishi nchini kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza hasa walimu wa sayansi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Novemba 29, 2021baada ya kuweka jiwe la msingi na kupata wasaa wa kuongea na wananchi na viongozi katika Shule ya Sekondari Kipoka wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, jumla ya walimu wa ajira mpya zilizopita kwa Mkoa wa Mbeya ulipelekewa walimu wapatao 336, lakini kwa nchi nzima uhaba wa walimu upo hasa kwa walimu wa sayansi na kwamba serikali itaendelea kutoa ajira hasa za walimu wa sayansi ili kupunguza upungufu wa walimu. 

Amesema, Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika Shule ya Sekondari Kipoka ili wanafunzi waweze kusoma wao wenyewe kwa vitendo bila kutegemea usaidizi kwa kiwango kikubwa.
“Upungufu tulionao mkubwa ni hasa walimu wa sayansi, lakini maabara ipo tutaleta vifaa pale kwa ajili ya maabara ya biolojia, kemia na fizikia ili kuwezesha wanafunzi 40 (kila maabara) wafanye majaribio wao wenyewe bila kukaa na mtu mwingine,”amesemema Mheshimiwa Majaliwa.  

Kuhusu ujenzi wa mabweni ya wanafunzi amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inao mpango madhuti wa kujenga mabweni ya shule za sekondari na kwa kuanzia yatajengwa mabweni ya wasichana na kisha mabweni ya wavulana ili wanafunzi waweze kusoma na kufanikiwa zaidi kitaaluma.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais (OR-TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amesema kwa nchi nzima Serikali imewezesha kujengwa madarasa 15,000 hapa nchini ambapo vyumba vya madarasa 12,000 ni kwa ajili ya sekondari na vyumba 3,000 ni vya shule shikizi za msingi.
Dkt.Dugange amesema, kwa Mkoa wa Mbeya, Serikali imepeleka shilingi Bilioni 12 na milioni 280 kwa ajili ya kujenga madarasa 464 sekondari na shule shikizi za msingi 164. 

Wilaya ya Chunya pekee 110 ambapo shule za sekondari ni vyumba vya madarasa 45 na shule shikizi vyumba vya madarasa 65. 

Ametoa pongezi kwa Mkoa wa Mbeya kuwa ujenzi wa vyumba vya madarasa unakwenda kwa wakati na matumizi ya bati nzuri hivyo ifikapo tarehe 15 Desemba,2021 huenda kazi yao itakuwa imekamilika na kukabidhiwa Serikalini.
Naye Mbunge wa Jimbo la Lupa, Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka ameiomba Serikali kuharakisha huduma ya maji katika Shule ya Sekondari Kipoka na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili wanafunzi na watumishi waweze kuendesha shughuli zao kwa urahisi, lakini pia ameomba kuongezewa idadi ya walimu kwa ajili ya kuboresha ufundishaji.

Post a Comment

0 Comments